27 December 2011

Hamad Rashid kikaangoni leo

*Kamati ya nidhamu, maadili kumuhoji na wenzake 12
*Wote watuhumiwa kukiuka utaratibu, katiba ya chama
*Ripoti ya mahojiano kuwasilishwa Kamati ya Utendaji
*Mtatiro: Njia aliyotumia haiwezi kukijenga chama chetu


Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeanza mchakato wa kumaliza mgogoro unaoendelea ndani ya
chama hicho ambapo leo, Kamati ya Nidhamu na Maadili itamuhoji Mbunge wa Wawi, Zanzibar, Bw.Hamad Rashid Mohammed, juu ya tuhuma alizozitoa hivi karibuni kupitia vyombo vya habari.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana kwa vyombo vya habari, imesema mbali ya kamati hiyo kumuhoji Bw.Mohammed, pia itawahoji wanachama 12 ambao wote wamepewa barua za kuitwa na kamati hiyo.

Mkuu wa Idara ya Nidhamu na Maadili ya chama hicho, Bw.Abdul Kambaya, alisema mahojiano hayo yatafanyika kwa siku tatu kuanzia leo hadi Desemba 29, mwaka huu.

Alisema kamati hiyo ilikutana juzi na kuazimia kuwaita watuhumiwa 13 akiwemo Bw.Mohammed na wanachama wenye nyadhifa mbalimbali katika chama ili wahojiwe kwa kosa la kukiuka utaratibu na katiba ya chama.

“Kesho (leo), tutaanza kumuhoji Bw.Hamad kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa sita, baada ya hapo tutamuhoji Bw.Juma Saidi Saanan (Mjumbe wa Baraza Kuu kutoka Unguja, Zanzibar), kuanzia saa sita hadi tisa alasiri na mwisho tutamuhoji Bw.Shoka Khamis Juma (Mjumbe wa Baraza Kuu kutoka Pemba, Zanzibar), kuanzia saa tisa hadi 12 jioni,” alisema Bw.Kambaya.

Aliwataja wanachama wengine ambao watahojiwa kuwa ni Bw.Doyo Hassan Doyo (Mjumbe wa Baraza Kuu kutoka Tanga), Bw.Yasini Mrotwa (Mjumbe wa Baraza Kuu kutoka Mbeya), Bw.Doni Waziri (Mwenyekiti wa Wilaya ya Ilala) na Bw.Mohamedi Massaga (Katibu wa Wilaya ya Ilala).

Wengine ni Bw.Albadawi (Mwenyekiti wa Wilaya ya Temeke), Bw.Amir Kilungi, Bw.Yusufu Mbungilo (Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Wilaya ya Temeke), Bw.Nanjase (Mwenyekiti wa Wilaya ya Nachingwea), Bw. Tamimu Omari (Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mkunduge, Kata ya Tandale) na Bw.Ahmed Issah kutoka Wilaya ya Morogoro Mjini.

“Kamati hii imeamua kuwaita kwa lengo la kujadiliana na kuangalia mustakabali wa chama chetu kwa mujibu wa katiba juu ya tuhuma zinazodaiwa na Bw.Mohammed pamoja na wanachama wengine 12 katika kipindi cha miezi miwili sasa,” alisema Bw.Kambaya.

Alisema baadhi ya wanachama hao wana makosa yanayofanana na wengine yanajitegemea ambapo baada ya mahojiano, kamati itapeleka taarifa kwenye Kamati ya Utendaji Taifa ya chama hicho ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kutoa maamuzi.

Aliongeza kuwa, kama kuna mwanachama ambaye hatakubaliana na maamuzi ya Kamati ya Utendaji, anaruhusiwa kukata rufaa katika Baraza Kuu la chama hicho.

Bw.Kambaya alisema, hadi sasa Bw.Mohammed hajapeleka tuhuma zozote katika chama kwa maandishi bali madai yake wanayasikia kupitia vyombo vya habari jambo ambalo ni kinyume na taratibu za chama hicho.

Aliwataka wanachama wa CUF, kuendeleza amani na utulivu hasa katika kipindi hiki cha vikao vya maamuzi ambavyo haviwezi kumuonea mwanachama yeyote.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Bw.Julius Mtatiro, alisema kitendo cha Bw.Mohammed kutotumia vikao vya chama ni utashi wake mwenyewe.

“Bw.Mohammed ameshindwa kutumia vikao, ndiyo maana wameamua kumuwahi, CUF inaendeshwa kwa taratibu na kanuni, kuna vikao vya chama ambavyo mwanachama anaweza kutoa hoja yake na wajumbe wakaikubali au kuikataa,” alisema.

Aliongeza kuwa, njia anazotumia Bw.Mohammed haziwezi kukijenga chama hicho ndiyo maana CUF imeamua kuchukua hatua za kumuita na kumuhoji.

Majira lilipomtafuta Bw.Mohammed ili kuthibitisha kama alipokea barua hiyo na kushindwa kuwasilisha tuhuma zake kwa uongozi wa chama, simu yake ya mkononi ilikuwa imezimwa.

Wiki iliyopita, Bw.Mohammed akiwa mkoani Tanga, alikanusha taarifa iliyoandikwa na gazeti moja linalotoka kila siku siyo (Majira) likimnukuu amekwenda kumuomba radhi Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ili asifutiwe uanachama na kupoteza ubunge.

Bw.Mohammed alidai kushangazwa na Maalim Seif kuendeleza malumbano katika vyombo vya habari na kukiuka agizo lake kuwa matatizo yote yanayotokea katika chama yafikishwe kwenye vikao si vinginevyo.

Alisema dhamira yake ni kupeleka tuhuma nne kwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba akimtuhumu Maalim Seif ili aweze kuchukuliwa hatua kwa madai ya kushindwa kusimamia shughuli za chama na kusababisha kipoteze mwelekeo.

Alizitaja tuhuma hizo kuwa ni pamoja na ofisi yake kushindwa kufanya kazi za chama upande wa bara na kusababisha chama hicho kishindwe vibaya katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.

Tuhuma nyingine ni matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za chama na ofisi yake kushindwa kutoa huduma stahiki kwa upande wa Bara na Zanzibar.

Bw.Mohammed alisema tuhuma ya nne ni chama hicho kushindwa kuutendea haki upande mmoja wa Jamhuri akitolea mfano katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Maalim Seif alishindwa kushiriki katika uzinduzi na ufungaji wa kampeni kwa upande wa bara.






2 comments:

  1. Hamad Rashid ameshamalizika kisiasa sasa hajui alitendalo

    ReplyDelete
  2. Hata maalim Seif naye kaisha hasa alipowekwe kinyumba na CCM.

    ReplyDelete