Na Zahoro Mlanzi
KATIBU Mkuu wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Joan Minja, ameteuliwa na Shirikisho la Kimtaifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kuwa
kamishna wa mechi kati ya Zambia na Botswana, itakayopigwa kati ya Februari 3,4 au 5, mwakani.
Mechi hiyo ni ya awali kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa Wasichana chini ya umri wa miaka 17, zitakazofanyika mwakani nchini Azerbaijan.
Hivi karibu Minja ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Ngumi la Ridhaa Tanzania (BFT) na Leslie Liunda, waliteuliwa kuwa wakufunzi wa waamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema mechi hizo zitafanyika kila kanda ambapo kwa Afrika fainali zake zitafanyikia nchini humo wakitafuta timu zikazoliwakilisha bara hilo.
“FIFA imemteua Joan Minja kuwa kamishna wa mechi hiyo mbapo katika tarehe hizo nchi mbalimbali zitashuka uwanjani zikiwemo Cameroon, Gambia, Ghana, Namibia, Nigeria, Sierra Lione, Tunisia na Afrika Kusini,” alisema Wambura.
Wakati huohuo, Wambura alisema leo na kesho kutakuwa na kozi ya makamishna wa Ligi Kuu Bara na ligi zingine zilizo chini ya TFF ambapo wanatoa wito kwa wale waliofanya Agosti, mwaka huu na hawakupita, wanaombwa pia kushiriki kwa mara nyingine.
“Kozi hiyo itakuwa ya siku mbili ambapo TFF inatoa nafasi nyingine hata kwa wale makamishna ambao katika kozi iliyopita hawakufanya vizuri waje kurekebisha makosa waliyofanya ili tuwe na wakufunzi wengi,” alisema Wambura.
Katika hatua nyingine, Wambura alizikumbusha timu za Simba na Yanga, kuhakikisha zinakuwa makini katika kupeleka majina ya wachezaji wao watakaowatumia katika michuano ya Afrika.
Alisema tayari tayari klabu hizo zimeshawasilisha majina yao ambapo Yanga imewasilisha majina 28 na Simba 24 huku kila timu ikihitajika kusajili wachezaji wasiozidi 30.
“Tunajua kila timu hapo baadaye katika usajili mdogo wa Agosti ina nafasi ya kuongeza wachezaji, lakini tunaziomba ziwe makini na vizuri kama zitakuwa na nafasi ya kuongfeza wachezaji wengine hapo baadaye,” alisema Wambura.
No comments:
Post a Comment