19 December 2011

Pinda: Tutachukua hatua kulinda viwanda vyetu

*Ahoji iweje juisi itoke nje wakati TZ ina matunda

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, amesema Serikali itachukua hatua za haraka kulinda viwanda vya ndani na kuzalisha bidhaa bora ili kuondoa kasumba ya
Watanzania kuthamini bidhaa za nje na kudharau za ndani.

Bw. Pinda alisema hayo Dar es Salaam juzi usiku katika hafla ya utoaji Tuzo za Rais Mwaka 2011 kwa Wanachama wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI).

Alisema anasikitika kuona fedha za kigeni zikitumika kununulia juisi nje ya nchi wakati Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, kuna mananasi ya kutosha ambayo yanaozea shambani.

Alisema Mkoa wa Tanga nao una machungwa mengi pamoja na maembe ambayo yanalimwa nchi nzima hivyo hakuna sababu ya juisi kuagizwa nje ya nchi.

“Hivi kweli kuna haja ya kuagiza siagi, asali, tomato (nyanya za kusindika) kutoka nje wakati malighafi tunazo nchini kwetu, hatuhitaji teknolojia ya ajabu au mtaji mkubwa ili tuweze kusindika vyakula na vinywaji hivi.

“Tunamtafuta Dkt. Nagu (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji), ili tuone tunaanzia wapi,” alisema.

Aliongeza kuwa, mazao ya kusindika yatawasaidia wakulima kuongeza thamani ya mazao yao na kukuza sekta ya kilimo ambayo inategemewa na Watanzania wengi hivyo kupunguza umaskini.

Bw. Pinda alisema, hatua hiyo itachangia ongezeko la ajira kwa vijana na nchi kutunza fedha za kigeni ambazo hutumika kuagiza juisi kutoka nje.

“Wadau watahusishwa kikamilifu katika maandalizi ya bajeti ya Serikali ili wajue vipaumbele na nafasi yao kwa uwazi zaidi, wawekezaji binafsi mnaruhusiwa kuzalisha kiasi chochote cha umeme badala ya megawati 10.

“Mchango wa sekta ya viwanda katika mauzo ya nje, umeongezeka kutoka asilimia 11.2 mwaka 2006, hadi kufikia 26.1 mwaka 2010, huku ajira ikiongezeka kutoka 90,210 hadi  109,545 kwa kipindi hicho,” alisema Bw. Pinda.

3 comments:

  1. Pinda nafikri naye ni mzigo wa nchi hii, KILA KITU IWE BUNGENI AU SEHEMU YEYOTE NI KUKOSA MAJIBU YA MAANA NA UTAFITI.HIVI ANAKUWA AMEALIKWA AJIANDAI KUSOMA MAPUNGUFU,MATATIZO NA MAFANIKIO NA SERA ILI AKIFIKA KWENYE UAMUZI ATOE DIRECTIVES SAHIHI,HII DHANA YA KUJIPANGA NI TAMTAFUTA FULANI, TUNAFANYA MCHAKATO ,NI UPUMBAVU

    ReplyDelete
  2. Ni jambo la kushangaza sana hivi hawa viongozi wanataka kutuambia ya kuwa hawajui siku zote ya kuwa nchi inaagiza juice tena kuto uarabuni kule jangwani na sisi tuna matunda ya kila aina na ardhi nzuri ya kuzalisha mazao mengi tu.Hii nchi ina mifano ya viongozi na sio viongozi ambao wanafikiria mambo ya maana.

    ReplyDelete
  3. Pinda alipaswa awaulize hao wenye viwanda ni kwa nini hawaanzishi viwanda hivyo hapa nchini huku mali ghafi ikiwa tele.
    Amuulize pia Bw. Mengi na Coca Cola, ni vipi kiwanda chao kiwe Kenya, na juisi iletwe hapa ikiwa tayari imekamuliwa, na sisi tuwapelekee matunda ya kukamua! Huo ni ukichaa!

    ReplyDelete