Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Mhandisi Martin Kitilla, amewataka wananchi kumpelekea kwa siri majina ya watendaji wa
mamlaka hiyo wanaodai rushwa ili wawahudumie.
Amewataka wananchi kuacha tabia ya kulalamika pembeni badala yake wachukue hatua ya kuwataja kwake watumishi hao wanaowaomba rushwa katika huduma zinazotolewa bure ikiwemo kubadili umiliki wa viwanja.
Mhandisi Kitilla alisema hayo juzi kupitia taarifa yake baada ya kuwepo kwa malalamiko ya wananchi kudaiwa rushwa ili kupatiwa huduma ya kubadili umiliki wa viwanja, mali zao na kuweka rehani (mortgage) ili kupata mikopo katika taasisi za fedha.
Katika taarifa yake Mkurugenzi huyo alisema, CDA inawataka wananchi kukataa kutoa rushwa ili kupatiwa huduma na baadhi ya watendaji na kusisitiza kuwa huduma hizo ni bure kwao.
"CDA inawataka wananchi wasilazimishwe kutoa rushwa wakati wa kupatiwa huduma ya kubadili umiliki wa viwanja au mali ili kupatiwa mikopo na taasisi mbalimbali, huduma hiyo ni bure," ilisisitiza.
Alisema kinachotakiwa kwa wananchi ni kuhakikisha wamelipa ada stahili za serikali na kutimiza masharti ya kuambatanisha nyaraka zinazohusika.
Alisema, mwananchi yeyote atakayedaiwa chochote kwa ajili ya kupatiwa huduma hizo atoe taarifa kwake au kwa kiongozi mwingine wa mamlaka hiyo na kwamba kwa kufanya hivyo watakuwa wamesaidia taifa kupunguza kero.
Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi mjini hapa, walionesha kufurahishwa na agizo hilo na kusisitiza kuwa licha ya juhudi zake za kutaka mabadiliko ndani ya CDA baadhi ya watendaji wake wanamsaliti.
Walisema watafikisha majina hayo kwake na kwamba baadhi yao wanaghushi nyaraka na kupora viwanja vyao na kufuta majina yao na kuingiza mengine.
No comments:
Post a Comment