16 December 2011

MUHAS yatimua wanafunzi

*Wahusishwa na vurugu zilizotokea chuoni

Na Godfrida Jola

CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kimewasimamisha masomo wanafunzi 66 kwa muda usiojulikana baada ya kufanya vurugu katika
mahafali chuoni hapo hivi karibuni.

Wanafunzi wengi waliosimamishwa ni wale wa mwaka wa tatu, tano na msichana mmoja ambao inadaiwa walipanga njama za kuvuruga sherehe hizo ambazo zilifanyika Desemba 10, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Kisali Pallangyo, alisema siku hiyo wanafunzi walianza kukusanyika katika jengo la utawala ili kuzuia mahafali hayo.

"Uamuzi wa kuwasimamisha wanafunzi hawa, umetolewa na Baraza la MUHAS baada ya kupata taarifa ya tukio hili na kulijadili kwa kina ambapo mchakato wa kuchukua hatua za kinidhamu zinaendelea," alisema Prof.Pallangyo.

Alisema katika madai yao ya msingi, wanafunzi hao walikuwa wakipinga ongezeko la posho za wabunge, kurejeshwa kwa Serikali ya wanafunzi chuoni hapo (MUHASSO) na kutoridhishwa na uongozi wa chuo.

"Wanafunzi hawa walivamia katika viti vilivyokuwa vimepangwa kwa ajili ya wahitimu hata walipoombwa kuondoka eneo hilo, walikaidi na wengine kuvunja viti," alisema.

Aliongeza kuwa, katika vurugu hizo polisi walilazimika kutumia nguvu na kuwakamata wanafunzi saba ambao walipelekwa rumande na mahafali hayo kufanyika chini ya ulinzi mkali.

Alisema Desemba 13, mwaka huu, masomo yaliendelea lakini kulikuwa na vitisho vya kutokea vurugu na kutishiana maisha hali ambayo baraza hilo lililazimika kufanya kikao cha dharura.

Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa chuo, Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Muhammed Bakari, alisema chuo hicho kinafuata sheria za Serikali na kuwataka wanafunzi kutumia njia za demokrasia kupata haki zao.

"Sisi kama utawala hatuamini kama wanafunzi wote ni wakorofi kwa sababu wamefika hapa kwa lengo la kujifunza, wakitaka haki zao wafuate sheria na taratibu," alisema.

Uongozi wa MUHASSO ulifutwa baada ya kukataa kutekeleza maagizo ya Serikali kupitia sheria namba 178 inayovitaka vyama vya wanafunzi katika vyuo vikuu nchini kurekebisha katiba zao kulingana na sheria ya vyuo vikuu namba 7 ya mwaka 2005.







No comments:

Post a Comment