28 December 2011

Mkwassa ataka tatu za kirafiki

Na Zahoro Mlanzi

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), ameliomba Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuitafutia timu hiyo mechi tatu za kujipima nguvu kabla
yaijaivaa Namibia.

Mechi hiyo ni ya kuwania kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake ambapo ya kwanza itachezwa jijini Windhoek, Namibia kati ya Januari 13, 14 na 15 mwakani na marudiano ni Januari 29 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Mkwassa alisema ni vizuri wakapata mechi tatu za nje ili kujiweka sawa kabla ya kucheza na wapinzani hao ambapo hata wakipata timu za Kenya na Uganda sio mbaya.

“Ikishindikana yote hayo basi hata wakicheza na timu za vijana za wanaume za hapa nyumbani, pia inaweza kuwasaidia kwani kikubwa ninataka kuona wachezaji wangu watakuwa katika kiwango gani,” alisema Mkwassa.

Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema timu hiyo itaingia kambini rasmi Januari Mosi ambapo ana uhakika mpaka kufikia siku hiyo watakuwa wamepata kambi ya kudumu.

Alisema kwa sasa timu hiyo inaendelea na mazoezi na kwamba wanafanya mazoezi wakitokea nyumbani na wakimaliza wanarudi makwao.

“Mchakato wa kutafuta mechi za kirafiki unaendelea ila kikubwa tunazidi kutoa wito kwa kampuni na taasisi kujitokeza kwa wingi kuisaidia timu hiyo kwani haina mdhami na ukiangalia kwa mfano gharama ya kupeleka timu Namibia si chini ya sh. milioni 50,” alisema Wambura.

Alisema ana amini kama timu hiyo itapewa motisha na kufanya maandalizi ya nguvu hana shaka itafika mbali na ikiwezekana hata kucheza robo fainali ya mashindano hayo.


No comments:

Post a Comment