19 December 2011

Maliasili yatupiwa lawama ugawaji vitalu

Na Said Njuki

WADAU wa uwindaji wa kitalii wa ndani na nje, wamezidi kuibana Serikali kwa kuituhumu Wizara ya Maliasili na Utalii kumilikisha vitalu vya uwindaji wa
kitalii kwa upendeleo.

Wakizungumza na Majira jana, wadau hao walisema ugawaji wa vitalu hivyo umefanyika bila kufuata taratibu na sheria hivyo kusababisha malalamiko mengi.

“Kimsingi haturidhiki na mchakato mzima uliotumika kugawa vitalu vya uwindaji licha ya maandalizi yake kufanyika muda mrefu kwa kuhusisha kamati maalumu,” walisema.

Uchunguzi uliofanywa na Majira, umebaini kuwa wizara hiyo imekuwa ikifanya mapitio ya ugawaji huo kwa kukutana na wadau waliolalamikia mchakato huo na kusikiliza malalamiko yao.

Imebainika kuwa, baadhi ya wadau hao wamepanga kujiondoa katika sekta hiyo kwa madai ya kunyang'anywa vitalu walivyokuwa wakivimiliki muda mrefu mbali ya kukidhi vigezo husika.

“Kimsingi sisi kama wadau wa ndani tulikuwa na matumani makubwa ya kupata vitalu vya uwindaji kwa sababu tumkidhi vigezo vyote vilivyotakiwa lakini hivi sasa tumekata tamaa ya kufanya biashara hii baada ya Wizara kutunyima vitalu tulivyoomba.

“Tumeanza mchakato wa kuangalia uwezekano wa kupata vitalu katika nchi nyingine kama Afrika ya Kusini, Zimbabwe na Malawi, kwani mchakato wa ugawaji umefanyika kwa siri, wapo waliokuwa wakimiliki vitalu zaidi ya vinne na kuvihudumia kwa hali na mali lakini nao wamenyang'anywa licha ya kutimiza vigezo,” walisema.

Baadhi ya wadau hao, wameiomba wizara hiyo kurudia mchakato upya na kama itashindwa, wapo tayari kwenda mahakamani kudai haki yao na wakishindwa kesi, watajiengua katika biashara hiyo.

Mdau mwingine alisema, baadhi ya masharti ya mzawa kupewa kitalu ni kuwa na uwezo wa kufanya shughuli za uwindaji lakini sharti hilo halikuangaliwa kwani zipo kampuni za wazawa zenye uwezo mkubwa ambazo zimenyimwa vitalu.

“Vitalu hivi havikugawiwa kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa ili kuleta tija kwa Taifa na jamii kwa ujumla, jambo la kushangaza wapo waliogawiwa vitalu hadi vinne, ukiangalia uwezo wao ni mdogo, labda wanataka kuingia mikataba na kampuni zenye uwezo ili wao waambulie ‘kamisheni’ kama baadhi ya kampuni zilivyokuwa zikifanya siku za nyuma,” alisema.

Alisema jambo muhimu ni nani ambaye ataendesha utalii wenye tija lakini siasa imechukua nafasi kubwa katika mchakato huo.

Katika kuhakikisha ugawaji vitalu unafanyika kwa uwazi na kufuata sheria, Mwaka 2008 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha azimio ambalo lilikusudia kuongeza uwazi katika ugawaji na umiliki wa vitalu vya uwindaji, maduhuli ya Serikali na ushiriki wa Watanzania wengi katika uwindaji wa kitalii, ambapo mwaka 2009 Bunge hilo lilipitisha Sheria mpya ya Wanyamapori Na. 5.


Utekelezaji wa azimio la Bunge, ilibidi uzingatie Sheria mpya ya Wanyamapori ambapo wizara hiyo iliandaa kanuni mpya za uwindaji wa kitalii zinazobainisha vigezo vya ugawaji vitalu na mwongozo ambao utakaotumika kutathmini waombaji vitalu hivyo.

Hivyo Sheria hiyo iliunda kamati ya kumshauri Waziri katika ugawaji wa vitalu, Kamati ya wataalamu ya kumshauri Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kuhusu aina na idadi ya wanyamapori watakaotumika kwa kipindi husika na kufanya tathmini ya kitaalamu ya vitalu vyote vya uwindaji wa kitalii nchini na kuviweka kwenye madaraja kulingana na ubora.

Akizungumzia madai hayo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Ezekiel Maige, alisema ni kweli baadhi ya wadau wameomba kuangaliwa upya mchakato wa uwagaji vitalu hivyo lakini hakuna taratibu, kanuni wala sheria iliyokiukwa katika ugawaji huo.

Alisema mdau ambaye hajaridhika na uwagaji huo, anaweza kwenda mbele zaidi kama mahakamani ili aweze kupaata haki.

“Nakuhakikishia hakuna Mtanzania aliyelalamikia ugawaji wa vitalu, baadhi wamelalamika kupewa vitalu ambavyo vipo maeneo ambayo hawakuyataka hivyo wakaomba warekebishiwe vitalu ili kurahisisha utendaji kazi wao.

“Chanzo cha tatizo ni baada ya kuwaondoa wageni (wazungu) kutokana na mabadiliko ya sheria si vinginevyo, kati ya kampuni 97 zilizomba vitalu, zilizolalamika ni asilimia 17 tu na zote ni za kigeni ambapo hicho ni kielelezo kuwa kazi ya ugawaji vitalu mwaka huu umekwenda kwa uwazi na haki kuliko miaka ya nyuma,” alisema Bw. Maige.

No comments:

Post a Comment