23 December 2011

JK ajionea athari za mafuriko Dar

*Aagiza waishio mabondeni kuhamishwa haraka
*Atembelea waathirika 4,909 waliopewa hifadhi
*Vifo zaidi vyaongezeka, sasa wafikia watu 20
*Dkt.Shein, CUF watuma salamu za rambirambi


Rais Jakaya Kikwete, akizungumza na waathirika wa mafuriko kwenye kambi iliyotengwa na serikali Mchikichini, Ilala, Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkuu wa mkoa Bw. Sadik Meck Sadik na Meya wa Ilala Bw. Jerry Silaa.
Na Waandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete amewaagiza viongozi wa Jiji la Dar es Salaam, kuhakikisha wananchi
waishio mabondeni wanahamishwa haraka ili kuwaepusha na maafa mengine yanayoweza kuwapata kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Agizo hilo amelitoa Dar es Salaam jana baada ya kufanya ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya jiji ambayo yameathiriwa na mvua kubwa zilizonyesha kwa siku tatu mfululizo na kusababisha maafa kwa wananchi hasa waishio mabondeni.

Mbali ya ziara hiyo, Rais Kikwete pia aliwatembelea waathirika 4,909 wa mvua hizo ambao wamepewa hifadhi katika Shule ya Msingi Mchikichini, iliyopo Manispaa ya Ilala.

Akiwa shuleni hapo, Rais Kikwete alisema Serikali imeguswa na maafa ya mvua hizo ambayo yamesababisha vifo, upotevu na uharibifu wa mali pamoja na miundombinu.

Alisema kama wananchi hao wataachwa waendelee kuishi katika maeneo hayo, Serikali italazimika kutumia fedha nyingi kuwahudumia kutokana na majanga wanayoweza kuyapata.

"Maafa kama haya yanasababisha nguvu kazi ya taifa ipungue hivyo jambo hili haliwezi kuvumiliwa, bahati nzuri viongozi wa jiji wapo hapa wananisikia," alisema.

Akiwasilisha ripoti ya mafuriko hayo kwa Rais Kikwete, Mkuu wa Mkoa huo, Bw.Meck Sadick, alisema hadi sasa vifo vilivyoripotiwa kutokana na mvua hizo ni watu 20.

"Katika vifo hivi, maiti 18 tayari zimetambuliwa na ndugu zao lakini maiti mbili, hazijatambuliwa na zimehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili."

Alisema kutokana na mafuriko hayo, tayari kuna ekari 2,000 ambazo zitapimwa na kupewa watu wanaoishi mabondeni ili waanze utaratibu wa kujenga na kuondoka maeneo hayo.

"Ekari hizi zipo katika Manispaa ya Kinondoni, ambapo viwanja vitapimwa na kukabidhiwa kwa watu zaidi ya 2,800, nawaomba watu ambao watapewa viwanja hivi wasiviuze kama walivyofanya awali baada ya Serikali kutoa viwanja katika maeneo ya Wazo Hill, Yombo na Kigamboni," alisema Bw.Sadick.

Mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw.John Mnyika, alisema upo umuhimu mkubwa wa jamii kutoa misaada mbalimbali kwa waathirika hao.

"Huu siyo wakati wa kulaumiana wala kuhusisha siasa, hili ni tatizo letu wote siyo wanaoishi bondeni pekee, mazingira ya kujiandaa kwa dharura bado duni sana kwa sababu kuna helikopta na boti ambazo zipo lakini hazikuweza kutumika katika janga hili," alisema.

Uchunguzi uliofanywa na Majira jana, ulibaini kuwa maeneo mengi ya jiji hilo jana yalianza kupitika kirahisi baada ya kupungua kwa maji yaliyoziba barabara.

Wamiliki wa nyumba zilizozingirwa na maji, jana walianza kuzifanyia ukarabati wa kawaida hasa kuziba kuta ambazo zilibomolewa ili maji yaliyoingia ndani yaweze kutoka kirahisi.

Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti, waathirika wa mvua hizo wameishukuru Serikali kwa kutoa msaada wa hali na mali jambo ambalo liliwafanya wafarijike mbali ya kupoteza mali za mamilioni.

Mmoja wa waathirika hao Bw.Frank Selebu, alisema licha ya kupewa hifadhi, wanahitaji vyandarua kwa ajili ya watoto ambao wanalala kwa shida hasa nyakati za usiku.

"Watoto wanaumwa na mbu usiku jambo ambalo linaweza kusababisha wapate malaria hivyo tunaiomba Serikali iwajibike kutupatia haraka," alisema.

Naye Bi.Rehema Alex alisema anasikitika kwa kupoteza samani zake zote hivyo aliishauri Serikali kuweka ulinzi katika maeneo yote yaliyokumbwa na mafuriko.

Alisema baadhi ya watu waliofika katika maeneo ya mafuriko hawakuwa na dhamira ya kuokoa wananchi bali walikwenda kuiba mali za waathirika.

Bw.Jackson John alisema usimamizi wa chakula wanachopewa siyo mzuri kwani baadhi ya waathirika wanarudia mara mbili na kusababisha vurugu.

Alisema lipo kundi la mateja ambao wanajifanya waathirika wa mafuriko hayo ili wapate misaada ya chakula na fedha.


"Hapa katika eneo ambalo tunahifadhiwa kuna idadi kubwa ya mateja ambao kama ukikaa vibaya wanakuibia wakijifanya waathirika wa mafuriko haya," alisema.

CUF watoa salamu za rambirambi

Chama cha Wananchi (CUF), kimetoa salamu za rambirambi kwa wafiwa waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki kutokana na mvua hizo.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Uenezi wa chama hicho, Bi.Amina Mwidau, alisema chama hicho kinawataka Watanzania wote waliopoteza ndugu na jamaa, wawe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Alisema CUF kinawapa pole Watanzania wote ambao nyumba zao zimebomolewa na mali zao kuharibiwa kutokana na mafuriko.

Bi.Mwidau alisema chama hicho kinatoa wito kwa kila Mtanzania kuchukua hatua ya kukabiliana na majanga hayo.

"Pamoja na kwamba Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), imekiri kuwa mvua hii haijawahi kutokea tangu mwaka 1954, bado Serikali ilikuwa na nafasi ya kupunguza madhara ya mvua hivyo, CUF tunaiomba ichukue hatua," alisema.

Alisema Serikali iwatafutie hifadhi wale wote ambao nyumba zao zimeathirika na hawana mahali pa kujihifadhi, kuwapa huduma za msingi na kuweka utaratibu mzuri wa wananchi kutoa msaada.

Chama hicho kimeitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, itoe maelezo ya kina  kwa nini imeruhusu baadhi ya wananchi kujenga mabondeni wakati historia inaonesha kuwa, maeneo hayo yamekuwa yanakawaida ya kutunza maji.

Alisema ni muhimu Serikali ikawajibika kwa kutoa majibu ya kuridhisha kwanini wameruhusu wananchi kujenga maeneo hayo.

"CUF inamtaka Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Dkt.John Magufuli kujifunza kutokana na mvua hizo na kutafuta namna ya kujenga barabara imara zenye uwezo wa kuhimili mvua kubwa." alisema

Alisema Serikali inapaswa kutumia vyombo vyake vya usalama, ujenzi na umeme kuhakikisha athari za mvua haziendelei.

Kutokana na maafa hayo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za pole Rais Kikwete.

Katika salamu zake, Dkt.Shein alisema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya mafuriko hayo na kusababisha baadhi ya watu kupoteza maisha na mali.

"Kwa niaba yangu binafsi na wananchi wa Zanzibar, natuma salamu za pole na rambirambi kutokana na watu waliopoteza maisha.

"Pia natoa pole kwa wananchi wote waliopata hasara kwa makazi yao kukumbwa na maji, kupoteza mali zao na kupata usumbufu mkubwa katika mafuriko haya," alisema.


Dkt.Shein alisema yeye na wananchi wa Zanzibar wanaungana na Rais Kikwete, ndugu na jamaa kuomboleza maafa hayo yaliyolikumba taifa.

"Namuomba MwenyeziMungu awarehemu wote waliopoteza maisha na awape subira wafiwa wote, nawaombea waathirika na wote wapate subira katika kipindi hiki kigumu."

Imeandaliwa na Salim Nyomolelo, Surah Mushi, Rahma Hamza na Peter Mwenda



1 comment:

  1. Poleni kwa waathirika wote, shukrani pia kwa viongozi waliojitokeza kusaidia!
    Kessy- Lusaka Zambia

    ReplyDelete