30 December 2011

CUF: Hamad Rashid tulimbana tuhuma 11

*Kamati yasisitiza zote alizikubali, akazitaka kwa maandishi

Na Rehema  Maigala

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema licha ya Mbunge wa Wawi, Zanzibar, Bw. Hamadi Rashid Mohammed, kukataa kuhojiwa na Kamati ya Nidhamu na
Maadili ya chama hicho, alikubali tuhuma zote 11 zinazomkabili.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Nidhamu na Maadili wa chama hicho Bw. Abdul Kambaya, alisema muda wa saa moja waliokaa na Bw. Mohammed kabla ya kukataa kuhojiwa, alikiri tuhuma hizo.

Alisema wakiwa ndani ya chumba cha mahojiano, Bw. Mohammed aliwasomea ujumbe anaodai ulitumwa kwa njia ya mtandao 'email' na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad na waraka wa Idara ya Ulinzi anaodai ulitumwa kwa Mwenyekiti wa chama Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba.

“Bw. Mohammed alikiri tuhuma zote alizosomewa zina ukweli lakini alikataa kuzijibu kwa madai hakuwa na imani na baadhi ya wajumbe wa kamati,” alisema Bw. Kambaya

Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo Bw. Mohammed aliomba kupewa tuhuma hizo kwa maandishi lakini kamati ilikataa kwa sababu kufanya hivyo ni kinyume na taratibu za chama.

“Tunamshangaa Bw. Mohammed kutokana na madai yake kuwa hana imani na Kamati ya Nidhamu na Madili lakini bado anahitaji tuhuma alizosomewa apewe kwa maandishi, huyu ni muasisi wa chama hiki, sijui kwa nini anataka kufanya vitu nje ya katiba na kusaababisha malumbano katika chama,” alisema Bw. Kambaya.

Alisema kesho (leo), chama hicho kitafanya kikao cha Kamati ya Utendaji ambacho kitakaa Zanzibar.

Majira lilipomtafuta Bw. Mohammed kwa njia ya simu ili kutoa ufafanuzi wa kile kilichosemwa na Bw. Kambaya alisema, hawezi kukubali kuhojiwa na kikao ambacho hakipo kikatiba.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimewatembelea waathirika wa mafuriko na kutoa msaada wa chakula, mafuta, maharage na nguo za aina mbalimbali.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Bw. Julius Mtatiro, aliongoza msafara huo ambao ulianzia katika kambi ya Shule ya Msingi Rutihinda, iliyopo Manispaa ya Kinondoni, Shule ya Sekondari Green Acres, Shule ya Msingi Mnazi Mmoja, Jangwani na Vingunguti.

Katika Manispaa ya Temeke, chama hicho kilitembelea waathirika waliopo katika kambi ya Shule ya Sekondari Kibasila na Shule ya Msingi Kingugi.

Akizungumza na waathirika hao, Bw. Mtatiro aliita Serikali itoe haki sawa kwa wamiliki wa nyumba zilizokumbwa na mafuriko hayo pamoja na wapangaji wao.

“Serikali itoe haki sawa kwa wenye nyumba na wapangaji ambao nao wanastahili kulipwa kwa kuwa wamepoteza mali nyingi katika mafuriko hayo,” alisema.

2 comments:

  1. Hamad Rashid Usalama wa Taifa na ingali anaitumikia kazi yake sasa naona imefika time ya kuivuruga CUF lakini jihadhari... maamuzi yaliochukuliwa yalistahili kuchukuliwa na kujiamini kwako eti unajua sheria zaidi unajidanganya........ Hamad Hakushinda jimboni kwake kwenye kura za maoni alipitwa na mtu mwenye elimu ya msingi mwaka 2005 na hatimae chama kilimnusuru kwa kurejesha uchaguzi ule..

    ReplyDelete
  2. Kiufupi Hamad Rashid alistahiki kufukuzwa kwenye chama kutokana na uasi wake. Nafikiri ni vyema sasa akagombea huko kwao KINONDONI ambako anakoishi. Mahakama ya kuu ya Tanganyika mwisho wake ni CHUMBE tu sio katika ardhi ya Waznzibari

    ReplyDelete