30 December 2011

Bundi bado aranda Yanga SC

Na Mwandishi Wetu

BUNDI bado anaonekana kurandi katika Klabu ya Yanga, baada ya jana baadhi ya wachezaji kuibuka na kudai kwamba, wanashangaa uongozi kushindwa kuwalipa
mishahara yao ya miezi miwili hadi sasa.

Akizungumza Dar es Salaam jana mmoja wa wachezaji wa klabu hiyo, ambaye hakupenda kuandikwa gazetini, alisema wanashangaa uongozi kushindwa kuwalipa wakati wana uhakika tayari wadhamini wao Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), imekuwa ikitoa fedha kila mwezi.

"Kwa kweli tunashangaa huu ni mwezi wa pili, hatujalipwa mishahara yetu wakati wenzetu Simba ambao nao wanalipwa na TBL wanacheka," alisema mchezaji huyo.

Alisema uongozi wa Yanga, unatakiwa kutafakari kwa kina kwa kuwa wao wanategemewa na familia zao, kwa kila kitu hivyo nyumbani hakukaliki kutokana na kukosa mahitaji muhimu.

Mchezaji huyo alisema hata mshahara wa mwisho waliopewa, walicheleweshewa kupewa kitu ambacho wanashindwa kuelewa ni nini kimetokea.

"Kwa kweli huko tunakokwenda sijui itakuwaje, tunakabiliwa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na pia tuna mechi ngumi ya Klabu Bingwa Afrika, dhidi ya Zamelek," alisema. 

Naye mmoja wa viongozi wa Yanga, ambaye hakupenda kutajwa jina lake kwa kuwa si msemaji wa klabu hiyo, alisema kuna tatizo limejitokeza kwani sasa hivi TBL hailipi moja kwa moja mishahara kama zamani.

"Tatizo ni kwamba mishahara siku tunalipwa na wakala aliyeteuliwa na TBL, lakini hata hivyo sielewi ni kwani nini wachezaji hawajalipwa kwa kuwa ninavyojua mshahara wa mwezi huu ndiyo tumecheleweshewa lakini iliyopita TBL ilishatoa sasa tatizo sijalijua bado," alisema.

Hali ndani ya Yanga, imekuwa si shwari tangu alipokaririwa na vyombo vya habari Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic ambaye alilalamika kwamba wana hali ngumu kifedha huku yeye akiwa asikilizwi kila anachokisema.

No comments:

Post a Comment