27 April 2011

Asakwa kwa kunyonga wanawe wawili

Na Mashaka Mhando, Tanga

MKAZI mmoja wa kijiji cha Misima wilayani Handeni mkoani Tanga, Mashaka Athumani (45), anasakwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuwanyonga watoto wake
wawili kisha kutokomea msituni baada ya kutokea ugomvi kati yake na mkewe.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa 7:00 usiku baada ya mkazi huyo ambaye kwa sasa anadaiwa yuko kwenye msitu mnene kati ya Sindeni na Kwamatuku, kufuatia mzozo kati yake na mkewe, Mwanaisha Gumbo.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Bw. Mohamed Jaffar  waliouawa ni watoto wa kike, Maseif Mashaka (2), na dada yake Amina Mashaka (7) aliyekuwa akisoma darasa la kwanza katika shule ya Msingi Misima. Watoto wengine watatu wa kiume walimkimbia wakati baba yao akinyonga hao wa kike.

Kamanda huyo alisema kuwa inavyosadikiwa ni kwamba muuaji alikuwa na mzozo baina yake na mkewe huyo kuhusu mali zilizoachwa na baba wa mwanamke huyo, Nassor Gumbo, ambapo mume huyo alikuwa akitaka agawiwe sehemu yake.

“Unajua taarifa ambazo tumezipata ni kwamba huyu muuaji alikuwa akiishi ukweni kwa mkewe hapo Misima, mkewe alifariki na kuacha kiasi cha mali ambazo mume yule anazitaka apewe kiasi kidogo na mkewe akamkatalia,” alisema kamanda huyo.

Alisema mwanaume huyo mara kwa mara alikuwa akileta mzozo na mwanamke huyo kutaka apewe fedha ili akafanyie biashara za madini katika migodi iliyopo katika wilaya hiyo, lakini mwanamke huyo alikuwa akimweleza kwamba hawezi kupata kwa vile hausiki katika mali ya baba yake mzazi aliyefariki.

“Baada ya kuelezwa hivyo mara kwa mara na mkewe, ndipo usiku wa jana (juzi) saa 7:00 usiku aliwaamsha watoto wake na kuwaeleza kwamba waondoke usiku ule wamfuate. Alipofika njiani akanza kumyonga yule mdogo aliyekuwa amembeba, kisha akamchukua dada yake Amina akamnyonga, watoto wengine wakiume walipoona baba yao anawanyonga wadogo zao walikimbia porini,” alisema Bw. Jaffar.

Alisema baada ya muuaji huyo kuwaua watoto wale aliwachukua na kwenda kuwaweka nje ya mlango nyumbani hapo kwa mkewe na kutokomea porini ambako anasakwa hadi sasa.

“Tutamkamata tu, maana hivi sasa askari wamesambaa katika msitu mkubwa wa maeneo ya Misima, Sindeni na Kwamatuku kumsaka na pia tunawatafuta watoto wake watatu ili tuwarejeshe nyumbani, watoto hawa wanaogopa pengine wanadhani baba yao yupo nyumbani na hivyo wakienda watanyongwa,” alisema.

Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili wameoneshwa kusikitsihwa na tukio hilo ambalo wamelielezea kwamba ni la kinyama na ambalo linapaswa kulaaniwa kwa sababu watoto wale hawahusiki na ugomvi kati ya baba na mama.

1 comment:

  1. Hivi sisi binadamu tumepatwa na shetani au ibilisi wa aina gani siku hizi?

    Mtu mzima na akili yako timamu unaua watoto malaika wa Mungu wamefanya kosa gani? Au ndiyo kumkomoa mwanamke, lakini mimi naona amejikomoa mwenyewe.

    Polisi tafadhali mtafuteni na mumuweke ndani huyo muuaji dhalimu wa roho za watoto wake mwenyewe. Na Mungu hatomwacha hivi hivi hata huko jela, tunamwombea ampe adhabu hapa hapa duniani kabla ya kufika huko akhera.

    ReplyDelete