20 December 2011

Acheni kuuza ardhi za wanyonge-CUF

Na Peter Mwenda

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Bw.Julius Mtatiro, amewaonya viongozi wa serikali za vijiji na kata wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani kuacha tabia ya
kuuza ardhi za wananchi wanyonge kinyemela kwa watu wenye uwezo.

Akihutubia wananchi wa Kata ya Msanga, Kisarawe, Bw.Mtatiro alisema amepata malalamiko ya wananchi kuwa watendaji wa kata wamekuwa wakishirikiana na viongozi wengine wa vijiji wa chama tawala kuuza mashamba ya wananchi kwa matajiri na wanapodai hawapati haki.

"CUF imepata taarifa za migogoro ya ardhi Kisarawe inayofanywa na Watendaji na Makatibu Kata wakishirikiana na viongozi wengine kuuza ardhi ya wananchi kwa watu wenye uwezo wanaobatizwa majina ya wawekezaji, naomba muache kuwanyanyasa wananchi maskini, msipotii tutawashughulikia," alionya Bw.Mtatiro.

Alisema kufanya hivyo ni kuwazidishia wananchi hali ngumu ya maisha na kwamba tatizo hili lipo karibu kila kona ya mkoa huo.

Alisema pia amepata taarifa za siri za baadhi ya watendaji wa kata katika mkoa huo kutaka kuzuia shughuli za CUF zisifanyike kwa kisingizio cha kuomba kibali.

"Mtendaji wa Kata ya Msanga jana usiku alizuia gari letu la matangazo lisitangaze mkutano wetu eti hatukuomba kibali, waambieni nchi hii ni ya Watanzania wote, tuna haki kama ilivyo CCM," alisema Bw.Mtatiro.

Alisema ni wakati mwafaka wa kuwakomboa Watanzania kuondokana na maisha mabovu waliyonayo na siyo kuzuia matangazo ya chama ambacho kimesajiliwa kihalali na kina haki zote.

Alitaka wananchi wa Kisarawe kuhakikisha wanaanza kukitupa nje CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 kama maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Bw.Mtatiro ambaye yuko katika ziara ya Mkoa wa Pwani akiwa Chalinze aliwaambia wananchi kuwa CUF imejipanga kuwaondoa Watanzania katika maisha ya umaskini uliokithiri kwa miaka 50 ya uhuru.



No comments:

Post a Comment