20 December 2011

Wizara ya Afya yazindua baraza la tiba asili

Na Salim Nyomolelo

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imezindua baraza linaloshughulikia masuala ya tiba asili nchini kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma hizo na kuondoa
kasoro zilizopo sasa.

Baraza hilo litaratibu na kusimamia usajili wa watoa huduma (waganga na wakunga), usajili wa vituo vya kutolea huduma, usajili wa dawa zinazotumika pamoja na usimamizi wa miiko na maadili ya tiba hiyo.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt.Hadji Mponda, aliwataka wajumbe wa baraza hilo kutambua na kuthamini kazi kubwa waliyopewa na serikali ya kusimamia wadau hao na kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

Aliwataka kutekeleza majukumu yao kwa  kuzingatia maadili ya tiba za jadi na uthabiti mkubwa bila hofu ya kuingiliwa katika maamuzi yao kwa masilahi ya wanataaluma na jamii kwa ujumla.

"Namshukuru na kumpongeza Dkt.Vuhaula Mpemba, ambaye ni Msajili wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, kwa kuiandaa shughuli hii, ambayo dhima yake ni kuzindua baraza jipya, pamoja na kuwapa mkono wa heri wajumbe waliomaliza muda wao katika baraza," alisema Dkt.Mponda.

Alisema tafiti zinaonesha kuwa takriban asilimia 60 ya wananchi wanatumia tiba asili katika kukabiliana na maradhi mbalimbali wanayoyapata na kwamba kiasi hicho cha wananchi siyo kidogo na kupuuzwa.

Alisema kila wilaya nchini iliteua mratibu wa tiba asili anayeratibu shughuli za tiba asili katika ngazi za wilaya ili kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi.

"Inakadiriwa kuwa kuna waganga na wakunga wa jadi wapatao 75,000 nchini, kwa hali hii ni muhimu kuwa na usimamizi wa karibu," alisema.

Aliongeza, juhudi hizo za serikali zinalenga kuhakikisha tiba asili inatumika kwa uwazi bila kificho na bila uwoga ikiwa ni pamoja na kuondoa dosari zilizopo.

"Nawaagiza mtumie sheria, kanuni na miongozo iliyopo ili kudhibiti wimbi la waganga wanaojitangaza katika vyombo vya habari.

Wanabandika matangazo mbalimbali kwenye mabango ambayo mengi yana matusi na hayapendezi kwa mila, desturi na utamaduni, mshirikiane na uongozi wa halmashauri kudhibiti hali hiyo," alisema.

Alisema tayari waganga na wakunga 2,050 pamoja na wasaidizi 379 walikamilisha kazi ya kulipia usajili na kwamba baraza lilifanikiwa kusajili waganga 434 hadi kufikia Septemba mwaka huu.



No comments:

Post a Comment