Na Zahoro Mlanzi
WANACHAMA na mashabiki 3,500 wa Klabu ya Yanga, wanatarajia kuhudhuria Kongamano la Vijana wa klabu hiyo, litakalofanyika Jumapili kwenye Ukumbi wa
PTA, Sabasaba jijini Dar es Salaam likiwa na lengo kutoa elimu kwa wana-Yanga hao.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo atakuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella.
Naye Mkufunzi wa Shirikisho Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Henry Tandau atatoa elimu ya soka huku Maofisa Ushirika wa Manispaa ya Ilala nao watatoa somo kuhusu SACCOS.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Kongamano hilo, Derick Msami alisema mchakato wa kufanya kongamano hilo ulianza tangu Novemba 14, mwaka huu baada ya vijana wa klabu hiyo kukutana na kujadili kwa kina suala hilo.
Alisema lengo kubwa la kongamano hilo ni kutoa elimu kwa vijana wote bila kujali kama ni mwanachama wa Yanga au la ili kuhakikisha wanajua jinsi klabu zinavyoendeshwa na mambo mengine.
“Kongamano hili limeandaliwa na Tawi la Yanga la Uhuru, jijini ambapo litatoa fursa kwa vijana kujitathimini kimaendeleo kwa kujua klabu ilipo na inapoelekea, kujiuliza ni jinsi gani walivyoisaidia klabu na si kila siku kulalamika klabu haijawasaidia kwanza wajiulize wenyewe,” alisema Msami.
Mbali na hilo, pia kongamano hilo litasaidia kuanzisha SACCOS ili iweze kusaidia vijana katika mambo mbalimbali na baadaye kuiendeleza kuwa na benki yao wenyewe jambo ambalo klabu itakuwa imepiga hatua kubwa.
Aliongeza kwamba kongamano hilo, linatakiwa liwe na watu zaidi ya 3,500 ambapo litaanza saa nne asubuhi mpaka saa 12 jioni.
No comments:
Post a Comment