09 November 2011

Waziri Mkuu awatia 'ndimu' Stars

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameichangia sh. milioni 10, timu ya Taifa Stars itakayocheza na Chad kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2014 mjini N’djamena ili ishinde.
Mchango huo wa Waziri Mkuu, ulikabidhiwa juzi wakati wa hafla ya kuiaga timu hiyo itakayoondoka leo kwenda nchini Chad.

Pinda alitoa fedha hizo kama motisha kwa wachezaji kufanya vizuri katika mechi hiyo ya michuano mikubwa duniani.

Alisema Tanzania atapenda kuona timu ikifanya vizuri na kusonga mbele hatua itakayofuata, katika michuano hiyo.

Waziri Mkuu aliwataka wachezaji wote kutimiza wajibu wao kwa kufuata maelekezo ya makocha wao. Stars inanolewa na Jan Poulsen.

“Mnakutana na timu nzuri, tunapenda kuona mkifanya vizuri na kufuzu hatua ya mbele zaidi, tafadhalini kachezani kwa kujituma na kupigana kwa ajili ya taifa lenu, ili muibuke na ushindi.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi aliungana na Waziri Mkuu kuwataka wachezaji wakajitume na kupigana mpaka dakika ya mwisho.

Malinzi aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, aliwataka wachezaji kuondoa tofauti za klabu zao na kuwataka kuwa kitu kimoja.

“Ninajua mnakutana na mechi ngumu, wanataka ushindi na sisi tunataka ushindi pia, wito wangu kwa wachezaji ni kucheza kwa kujituma, nitapenda kuona wachezaji wakirejea nyumbani wakiwa wamefungwa bendeji ngumu (POP) kwa ajili ya kulipigania taifa,” alisema Malinzi.

Kwa upande wake Kocha Mkuu Poulsen, alisema anafahamu wanacheza wakiwakilisha wananchi zaidi ya milioni 40, hivyo watajituma katika mechi hiyo ili waibuke na ushindi.

Poulsen alisema, wachezaji wote wako katika hali nzuri na wako tayari kupigania taifa pamoja na kumkosa mchezaji muhimu, Nadir 'Cannavaro' Haroub aliyeumia kifundo cha mguu mazoezini.

“Kiufundi tuna timu nzuri na tuna uhakika itawakilisha vizuri katika mechi hiyo, tuko tayari kwa ajili ya mechi,” alisema Poulsen.

Nahodha wa timu hiyo, Joseph alimshukuru Waziri Pinda kwa mchango wake na kuwahakikishia Watanzania kuwa, watajituma katika mechi hiyo.

“Tunajua wajibu wetu na tuna imani tutashinda kwenye ardhi ya ugenini na baadaye kwenye ardhi yetu,” alisema Joseph.

Kikosi hicho cha Stars kitaondoka leo jioni kikiwa na makipa, Juma Kaseja, Mwadini Ally.

Mabeki ni Godfrey Taita, Juma Jabu, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Juma Nyoso na Idrissa Rajab.

Kwa upande wa viungo ni Henry Joseph, Ramadhan Chombo, Nurdin Bakari, Shabani Nditi, Abdi Kassim na Shomari Kapombe.

Washambuliaji ni Nizar Khalfan, Mrisho Ngassa, John Boko, Mbwana Samata, Athuman Machupa, Hussein Javu na Thomas Ulimwengu.

2 comments:

  1. Tatizo kubwa la timu yetu ni maandalizi duni,Hatuwezi kufanya kitu cha maana kwa maandalizi duni.Waangalie Zanzibar leo hii wamekwenda kupiga kambi Misri sasa kama wao wameweza kwanini Tanzania bara isiweze?,Hakuna ushindi unaokuja kirahisi bili ya maandalizi ya kutosha.Tunatecheza na dj'buti na wao wamepiga kambi Tunisia wiki mbili zilizipita.Sasa hivi tunatakiwa tuache maandalizi ya zimamoto.Tangu aondoke Maximo hakuna Program maalum iliyoandaliwa kwa ajili ya vijana wadogo ambao wanaweza kutayarishwa kwa ajili ya timu ya taifa ya vijana.Kazi yetu kubwa ni kung'ang'ana na vijeba ambavyo unataka kuvifundisha mambo ambayo walitakiwa kufundishwa udogoni.Serikali inatakiwa kuelewa ya kuwa inatakiwa kuwakeza kwa vijana wadogo alafu matunda yataonekana baadae na sio staili hii tulionayo.

    ReplyDelete
  2. Samahani tunacheza na Chad

    ReplyDelete