NEW York, Marekani
BONDIA ambaye ni bingwa wa zamani wa ngumi za uzito wa juu duniani, Joe Frazier amefariki dunia baada ya kupambana na kansa ya ini, familia yake imesema.
Frazier ambaye alikuwa akijulikana kama 'Smokin' Joe, alikuwa akipata tiba Philadelphia baada ya kugundulika kuwa na kansa wiki kadhaa zilizopita.
Joe amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 67, wakati wa uhai wake aliwahi kuwa wa kwanza kumtwanga bondia maarufu wa zamani Muhammad Ali mwaka 1971, lakini alikuja kurudiana naye katika mapambano mawili baadaye ambayo yote alipigwa dhidi ya Ali.
Alikuwa bingwa wa dunia katika miaka ya 1970 na 1973.
Alitwaa ubingwa wa dunia mwaka 1970 kwa kumtwanga Jimmy Ellis mjini New York. Miaka mitatu baadaye alipoteza ubingwa huo kwa kupigwa na George Foreman.
Jumamosi aliyekuwa Meneja wa Frazier, Leslie Wolf alisema kuwa hali ya bondia huyo ilikuwa mbaya sana, lakini madakatari na timu ya Frazier wanajitahidi kufanya kila kitu wanachoweza.
Frazier enzi za uhai wake, wakati akipigana katika ridhaa alitwaa ubingwa wa Olimpiki na kutwaa medali ya dhahabu mwaka 1964.
Medali hiyo akitwaa alipokwenda kwenye mashindano hayo kama mchezaji wa akiba kuziba nafasi ya Buster Mathis, ambaye alimpiga katika mechi za kuwania tiketi ya kucheza mashindano hayo, lakini alishindwa kwenda kutokana na kuumia.
Frazier anajulikana zaidi kwa mapambano yake matatu aliyopigana na Ali wakati wa uhai wake, likiwemo lililojulikana kama "Thrilla in Manila" mwaka 1975.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uongereza (BBC), baada ya kusikia hali ya ugonjwa wa Frazier, Ali (69) alisema: " Habari kuhusu Joe ni ngumu kuamini na ngumu zaidi kukubali."
"Familia yangu inaungana na familia ya Joe, katika sala za kila siku. Joe ana marafiki wengi, mimi ni mmoja wao," alisema Jumapili.
Frazier alistaafu ngumi mwaka 1976, baada ya kupigwa na Foreman. Kisha alijaribu kurejea tena ulingoni 1981, ambapo alipigana mara moja na kustaafu moja kwa moja.
Historia fupi ya Frazier alizaliwa Januari 12, 1944 Beaufort, South Carolina.
Alipigana mapambano 37, alishinda 32 (27 kwa KO), alipigwa mara nne na sare moja.
Alitwaa medali ya dhahabu kwa Marekani katika Mashindano ya Olimpiki, Tokyo 1964.
Pia alitwaa ubingwa wa NYSAC (wa dunia) kwa kumpiga, Buster Mathis 1968.
Alitwaa ubingwa wa dunia wa uzito wa juu WBA na WBC akimshinda Jimmy Ellis mwaka 1970. Ubingwa wake wa mwisho aliutwaa 1975, alipopigana na Muhammad Ali.
Alistaafu ngumi 1976 na akarejea tena ulingoni 1981, alipigana mara moja kabla ya kustaafu moja kwa moja. Alifariki juzi baada ya kuugua kansa.
No comments:
Post a Comment