Na waandishi maalumu
Wanariadha 30 wanaokimbiza bendera ya taifa, kupitia kampeni ya Kilimanjaro Jivunie uTanzania inayoenda sambamba na
sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, jana wameagwa jijini Dar es Salaam.
Akiwaaga wanariadha hao, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadiki, aliwapongeza kwa kuwa wazalendo na kukubali kuikimbiza bendera mpaka kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Pia aliipongeza Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager kwa kubuni mbio hizo za bendera, huku akizipa changamoto kampuni nyingine kuiga mfano huo.
“Hizi ni sherehe kubwa za kizalendo na kuna kampuni nyingi zenye uwezo, lakini TBL imeonesha uzalendo mkubwa san tulitegemea wengi wangejitokeza, lakini hawa wameonesha mfano,” alisema.
Wanariadha hao wameondoka na bendera ya bluu ambapo wataungana na wanariadha wengine 60 kutoka Mwanza, Dodoma na Arusha wanaobeba bendera za njano, nyeusi na kijani.
Baadaye wanariadha hao wataungana na wenzao mjini Moshi na kuunganisha rangi zote, ili kupata bendera moja ya taifa itakayopandishwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Akizungumza Dar es Salaam jana Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe aliwataka wananchi kuwasubiri wanariadha hao na kuwapokea kama mashujaa, kwani wameonesha uzalendo wa hali ya juu.
“Tayari wameshapokewa katika maeneo kama Kondoa na Bunda kama mashujaa kwa hivyo hata hawa wanaoondoka nawaomba wananchi wawasubiri na kuwapokea kama mashujaa kote watatakopita,” alisema.
Kampeni ya Jivunie uTanzania ilizinduliwa Julai 5, mwaka huu kwa lengo la kusherekea miaka 50 ya Uhuru na kuwakumbusha Watanzania mafanikio yaliyopatikana katika miaka 50 ya Uhuru.
No comments:
Post a Comment