Na Zahoro Mlanzi
JUMLA ya wagombea wanane kutoka nchi mbalimbali za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambao ni wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu vya ukanda
huo (CECAFA), wanaowania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji wa baraza hilo wametajwa.
Uchaguzi Mkuu wa baraza hilo unatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Novemba 24, mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema kama ilivyotangazwa awali Mwenyekiti wa baraza hilo, Leodegar Tenga atatetea nafasi hiyo akichuana na Makamu wake Fadoul Hussein, kutoka Djibouti.
Alisema nafasi nyingine ni ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambayo inawania na wagombea wanane ambao ni Abdiqani Saeed Arab wa Somalia, Tariq Atta Salih (Sudan), Justus Mugisha (Uganda) na Tesfaye Gebreyesus (Eritrea).
"Wengine ni Hafidh Ali Tahir (Zanzibar), Sahilu Wolde (Ethiopia), Raoul Gisanura (Rwanda) na Abubakar Nkejimana (Burundi) ambapo kati yao wanahitajika wanne kuingia katika kamati hiyo," alisema Wambura.
Wakati huohuo, Wambura alizungumzia pia kozi ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kwa ajili ya waamuzi watakaochezesha mashindano ya CECAFA Tusker Chalenji Cup, itafanyika Novemba 22, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Aliwataja waamuzi walioteuliwa na CECAFA kuchezesha mashindano hayo ni Dennis Batte (Uganda), Bamlak Tessema (Ethiopia), Davis Omweno (Kenya), Wish Yabarow (Somalia), Israel Mujuni (Tanzania), Munyemana Hudu (Rwanda), Eric Gasinzigwa (Burundi) na Garvis Munyenziza (Rwanda).
Wengine ambao ni waamuzi wasaidizi ni Hassan Egueh (Djibouti), Clemence Erasmo (Tanzania), Idam Hamid (Sudan), Juma Ali Kombo (Zanzibar), Hamis Chang'walu (Tanzania), Yohanes Girmai (Eritrea), Brazan Mamati (Kenya), David Sagero (Kenya) na Mark Sonko (Uganda).
Aliongeza kwamba waamuzi wote wa Tanzania, wenye beji za FIFA nao watashiriki katika kozi hiyo.
No comments:
Post a Comment