22 November 2011

Boban amchefua Julio

*SMG, Mgosi waitwa Kili Stars

Na Zahoro Mlanzi

PAMOJA na kupewa nafasi katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), mshambuliaji Haruna Moshi 'Boban' amemchefua Kocha Msaidizi wa
timu hiyo, Jamhuri Kihwelu 'Julio' ambaye amempa saa 24 awe ameingia kambini la sivyo atakuwa amejifukuzisha mwenyewe.

Boban na Gaudance Mwaikimba, ndiyo wachezaji pekee ambao kwa kiasi kikubwa walikuwa wakipigiwa chapuo kuwepo katika kikosi cha timu hiyo, lakini Mwaikimba amejiunga na wenzake ila ugumu umebaki kwa Boban.

Mbali na hilo, Julio amewaongeza katika kikosi chake wachezaji Mussa Hassan 'Mgosi' na Said Maulid 'SMG' badala ya Nizar Khalfan na John Bocco.

Akizungumza Dar es Salaam jana asubuhi, wakati wa mechi za Uhai Cup zinazoendelea kwenye Uwanja wa Karume, Julio alisema leo anatarajia kufanya mchujo wa wachezaji sita kati ya 28, aliowateuwa kwa ajili ya michuano ya Kombe la Tusker Chalenji.

"Kikosi changu kinaendelea vizuri na mazoezi na wachezaji wote wameshaingia kambini isipokuwa Boban, Nizar na Bocco ambaye ameumia hivyo nafasi yake itachukuliwa na Mgosi," alisema Julio.

Alisema amejaribu kuwasiliana na Boban kwa nyakati tofauti, lakini majibu aliyopewa ni kwamba ana udhuru na yupo Arusha, hivyo atakaporudi atajiunga na wenzake kambini.

"Mimi ni zaidi kuliko yeye (Boban), nasemaje kama hajafika mpaka kufikia leo (jana) jioni, atakuwa amejiondoa katika kikosi changu kwani hatuwezi kufanya kazi kwa mtindo huo," alisema Julio.

Akizungumzia suala la Nizar, alisema mpaka sasa hana uhakika kama mchezaji huyo atakuja, hivyo kutokana na hilo ameamua kumwongeza SMG, akitengeneza mazingira kwa lolote litakalotokea juu ya Nizar.

Julio pia awaomba Watanzania kuwa na umoja na ushirikiano hususani wakati wa mashindano, kwani hiyo timu si ya watu wachache ni ya Watanzania wote.

Kili Stars itaanza kampeni za kutetea ubingwa wake kwa kuumana na Rwanda 'Amavubi' katika mchezo utakaopigwa Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment