08 November 2011

Vodacom: Wateja kupiga kura bure Mlima Kilimanjaro

                
Na Nickson Mahundi
KAMPUNI ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania imetoa nafasi ya bure kwa wateja wake nchi nzima kushiriki katika kuupigia kura Mlima Kilimanjaro na kuuwezesha kushinda kuingizwa katika orodha ya maajabu saba mapya ya dunia.

Ofisa Masoko Mkuu na Mahusiano wa Vodacom Tanzania Bi.Mwamvita Makamba alisema wajibu na jukumu la kuuwezesha Mlima Kilimanjaro kushinda ni letu, hivyo tuungane pamoja kama taifa na Vodacom inatoa fursa adhimu kwa Watanzania kuuwezesha  Mlima huo ambao ni fahari ya Tanzania kushinda na kuongeza sifa na kuendeleza heshima ya Tanzania katika ulimwengu.

Ili kushiriki mteja wa Vodacom anahitajika kutuma BURE ujumbe mfupi wa neno 'KILI' au KILIMANJARO kwenda namba 15771 kuanzia leo hadi  Novemba 17, 2011.

“Ni wakati wa kuonesha uzalendo wetu Vodacom inatoa fursa hii ya kipekee, kila mmoja aweke simu yake ya Vodacom wazi na apige kura, ni Imani yangu na ya Vodacom kwamba kwa nafasi hii isiyo na gharama Mlima Kilimanjaro utashinda tukitambua kwamba kila nchi inapigania kushinda moja ya nafasi saba zilizotangazwa.”alisema

Vodacom inaungana na  Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Watanzania kwa ujumla kuhamasisha wananchi kushiriki kwa wingi katika kuupigia debe mlima Kilimanjaro kwa masilahi ya taifa.

“Kwa sasa Bonde la Ngorongoro linatuwakilisha katika orodha ya maajabu saba ya ulimwengu ambayo na hilo limetuletea sifa kubwa kama taifa, hivyo kwa kufanikiwa kuuongeza Mlima Kilimanjaro ambao ni mlima mrefu kuliko yote barani Afrika kutaongeza sifa ya nchi mbele ya sura ya dunia sambamba na kukuza pato la taifa litokanalo na sekta ya utalii,”alisema






  

1 comment:

  1. SAWLI: Je wadu walioko nje ya nchi wapige kura vp kuongeza vote? Naomaba majibu kwa ajuae

    ReplyDelete