08 November 2011

TPSF yaanda mkutano wa wafanyabishara

Na Nickson Mahundi
TAASISI  ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) imewashauri  wafanyabishara   nchini kujitokeza  kushiriki katika mkutano unaotarajia kufanyika kesho kutwa kwa kushirikiana na wengine  kutoka Singapore.
Ushauri huo  ulitolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Bi. Esther Mkwizu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio huo wa wafanyabishara 26 ambao utaongozwa na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Singapore.

“Mkutano huu ni muhimu sana kwetu tunawaomba wafanyabiashara wa Tanzania kuhudhuria bila kukosa ili kuweza kukutana wenzao  na kubadilishana mawazo na kujenga mtandao wa kibiashara miongoni mwao,”alisema

Alisema Singapore imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya uhandisi, mawasiliano ya simu, teknolojia ya habari na mawasiliano (TEKNOHAMA), kilimo, nishati, ujenzi, usafirishaji, uvuvi, afya, elimu na madini hivyo ni fursa kwa watanzania wanaotaka kupata washirika kuwekeza kwa ushirikiano katika maeneo hayo.

Alisema katika mkutano huo pia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA) wanatarajia kuwasilisha mada kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Ujumbe huu pia utakutana na Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw.Mustafa Mkulo; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Cyril Chami na pia utatembelea Makao makuu ya Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA) na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Adelhelm Meru.

Mkuu wa Idara ya Fedha wa kampuni ya Singapore inayofanya kazi hapa nchini ya Olam Tanzania, Bw. Anand Saboo alisema ujio wa wafanyabiashara hao ni fursa muhimu kwa Tanzania kwa kuwa nchini hiyo imepiga hatua katika masuala mbalimbali ya maendeleo.

Alisema ujio huo ni fursa kubwa kwa yeyote anayetaka kufanya biashara na makapuni ya Singapore ambapo ujumbe huo utanadi maeneo zaidi ya kumi ambayo ni muhimu kwa ushirikiano wa biashara na uwekezaji.


  

No comments:

Post a Comment