Na Theonestina Juma, Bukoba
IDADI ya watu waliofariki katika ajali ya barabarani iliyohusisha basi la abiria na garila mizigo kwa kugongana uso kwa uso imeongezeka kutoka 16 hadi 18. Habari zilizopatikana
mjini hapa na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Bw. Henry Salewi, zimeeleza kuwa idadi hiyo imeongezeka baada ya majeruhi wawili kufariki jana asubuhi katika hospitali Teule ya Wilaya ya Biharamulo mkoani hapa.
Kamanda Salewi alisema katika ajali hiyo iliyotokea juzi saa 4.30 asubuhi katika barabara ya Rusahunga Nyakahura watu 11 walifariki papo hapo huku wengine saba wakifia hospitalini.
Alisema katika ajali hiyo ambayo chanzo chake inadaiwa kuwa ni mwendo kasi na madereva wote wawili kutokuwa waangalifu ilihusisha basi la Kampuni ya Taqwa aina ya Nissan T 635 AVC iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Bujumbura nchini Burundi na lori RAB 255 ACT mali ya kampuni ya Azam iliyokuwa ikitokea nchini Burundi.
Kamanda Salewi alisema katika ajali hiyo watu 18 waliofariki, wanane
wametambuliwa kwa majina na watano kati yao kuchukuliwa na ndugu zao, miili mitatu ikisubiri kuchukuliwa huku maiti 10 zikiwa bado hazijatambuliwa kabisa.
Aliwataja waliotambuliwa kuwa ni pamoja na dereva wa basi la Taqwa, Bw. Sultan Mohamed (36) mkazi wa Kahama mkoani Shinyanga, dereva wa lori Bw. Ruzindana Theonest (35) mkazi wa nchini Rwanda, Herick Heliud ( 18) mkazi wa wilayani Ngara.
Aliwataja marehemu wengine kuwa ni pamoja na Chinuka Amajata (25-35) mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye ni raia wa Zambia, Bi. Farida Abdallah (35) mkazi wa Tabora.
Wengine ni pamoja na Bi. Habiba Juma (45),Bi. Aziza Said (60) wote wakazi wa Tabora na Bw. Ally Issa (35) mkazi wa Dar es Salaam.
Aliwataja majeruhi 17 waliotambuliwa kuwa ni pamoja Bw. Joseph Baltazar (24), Bw. Donald Kichaa, Bw. Pineer Elisha (12), Anjinta Sewitta (53), Bw. Samuel Rusulo (46) wote wakazi wa wilayani Ngara, na mtoto Said Suleman (4).
Wengine ni Mutabenda Anceth (29), Bw. Kabula Ismael (27), Bw. Joseph Bugiriman (34) wote wakazi wa Burundi, Bi.Jane Kassag (46), Bw. Andongwisie Makikisisire (39) Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Bw.Abeid Dafulla wote wakazi wa Dar es Salaam.
Alisema kati ya majeruhi hao 17 watano hawajatambuliwa majina kutokana na kuwa katika hali mbaya na kwamba wote wamelazwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Biharamulo na Murugwanzwa wilayani Ngara. Alisema miili ya marehemu wa ajali hiyo imehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Biharamulo.
No comments:
Post a Comment