22 November 2011

Utetezi kesi ya samaki wa Maguli yafungwa

Na Rehema Mohamed na Zena Mohamed

UPANDE wa utetezi katika kesi ya uvuvi haramu ndani ya Bahari ya Hindi kwenye kina kirefu cha Ukanda wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania maarufu kesi ya ‘Samaki wa Magufuli'
umefunga ushahidi wao.

Upande wa utetezi ulifunga ushahidi wao jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Profesa Agustina Mwarija, anayesikiliza kesi hiyo.

Kutokana na hali hiyo mawakili wa pande zote mbili wametakiwa kuwasilisha hoja kama washtakiwa wana hatia au la Novemba 29 mwaka huu.

Hoja hizo zinatarajiwa kuwasilishwa kwa njia ya mdomo mahakamani hapo baada ya kukamilika kwa kusikilizwa kwa utetezi kwa pande zote mbili.

Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri unawakilishwa na wakili Biswalo Mganga huku miongoni mwa mawakili wa upende wa utetezi ni Bw.Ibrahim Bendera.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Bw. Zhao Qinj ambaye ni wakala wa meli ya Tawariq 1 inayodaiwa kubeba samaki hao, manahodha wa meli hiyo Bw. Hsu Shang Pao, Bw.Ca’ Dong Li na Chen Rui Hai.

Machi 9 mwaka 2009 washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa ya uvivu haramu katika kina kirefu cha bahari ya Hindi Ukanda ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuharibu mazingira ya ukanda huo.

Washtakiwa hao walikamatwa katika operesheni ya kulinda rasilimali za Tanzania iliyokuwa ikiendeshwa na serikali kupitia Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa wakati huo Dkt. John Magufuli.

No comments:

Post a Comment