22 November 2011

Majambazi wateka mabasi matatu

Na Moses Mabula, Tabora

MAJAMBAZI sita wakiwa na bunduki pamoja na mapanga, wameteka mabasi matatu yaliyokuwa yakitokea Jijini Dar es Salaam kwenda Tabora na kupora mali pamoja na
pesa za abiria sh. milioni tatu.

Tukio hilo lilitokea juzi saa mbili usiku katika Kijiji cha Tuli, Kata ya Ndevelwa, Manispaa ya Tabora ambapo majambazi hayo baada ya kufanya utekaji huo, yaliwalazimisha abiria wote waliokuwa ndani ya mabasi hayo kuvua nguo kabla ya kufanya uporaji.

Mabasi yaliyotekwa ni Muro Investments lenye namba za usajili T937 BFW, NBS na Air Bus.

Akizungumza na Majira jana, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Antony Rutta, alisema mabasi hayo yalitekwa umbali wa kilometa 20 kutoka mjini Tabora pamoja na pikipiki moja inayofanya biashara ya 'bodaboda', yenye namba za usajili T 233 aina ya Sunlg.

“Hawa majambazi waliweka magogo barabarani hivyo mabasi haya yalishindwa kupita, basi la kwanza kutekwa lilikuwa la Kampuni ya Muro ambalo baada ya kufika eneo hilo, lilishambuliwa kwa risasi.

Kamanda Rutta alisema, basi la pili kutekwa lilikuwa Air Bus lakini askari wawili waliokuwa katika basi la NBS baada ya kufika eneo hilo, walipambana na majambazi hao.

“Hawa majambazi walizidiwa nguvu na kulazimika kukimbia, jambazi mmoja mwanaume alipigwa risasi na kufariki muda mfupi baadaye na hadi sasa, bado hajatambuliwa.

“Hajulikani ni mkazi wa wapi na baada ya kupekuliwa, alikutwa na simu mbili ambazo zilikuwa za abiria waliotekwa, hawa asjari ni PC Joseph mwenye namba G. 4260 na D/C Deogratius mwenye namba G. 4429,” alisema Kamanda Rutta.

Alisema wakati basi la NBS lilipofika eneo hilo, majambazo hao walikuwa wakiendelea kukusanya mali za abiria.

Aliongeza kuwa, awali majambazi hao walimteka mwendesha pikipiki ya abiria 'bodaboda', Bw. Masi Wiliam (24), ambaye walimpora sh.  18,000.

Pikipiki hiyo ilikutwa eneo la tukio baada ya askari hao kupambana na majambazi ambapo Bw. Wiliam, alikwenda Kituo cha Polisi mjini humo kutoa taarifa.

1 comment:

  1. ongereni sana askari wetu na jeshi liwaangalie kwa motisha,pia wenye mabasi acheni uzembe hakikisheni kwamba mnakuwa na askari"escort"

    ReplyDelete