Na Zahoro Mlanzi
KAMATI ya Uchaguzi ya Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT), imepanga kufanya Uchaguzi Mkuu Aprili 24, mwakani. Awali uchaguzi huo ulipangwa kufanyika mapema mwaka
huu, lakini baadaye ikabainika katiba itakayowaweka madarakani viongozi wapya, ina upungufu hivyo ifanyiwe marekebisho kisha ndiyo uchaguzi ufanyike.
Kamati hiyo ilisimamia suala hilo kwa kufanya mkutano wa dharura uliofanyika Dodoma mwezi uliopita, ambapo kwa pamoja walifanya marekebisho hayo na kuweka vifungu vipya.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa chama hicho, Alhaj Muhidin Ndolanga alisema mchakato wa kupata viongozi kwa ngazi zote kuanzia wilaya, mpaka taifa umeshaanza tangu Jumamosi.
"Kwa mujibu wa kile kikao cha marekebisho ya katiba, tulikubaliana kwamba mchakato wa kupata viongozi wa wilaya, uanze Novemba 20, mwaka huu mpaka Januari Mosi mwakani," alisema Ndolanga.
Alisema kwa upande wa mkoa, mchakato huo utaanza Januari 13 mpaka Machi 2, wakati ule wa taifa utaanza Machi 3 mpaka Aprili 27, hivyo baada ya kukamilika kwa zoezi kila ngazi itakuwa na viongozi wapya.
Alizitaja nafasi zitakazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Msaidizi wake, Mhazini na Msaidizi wake pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
Aliongeza kwamba katika kila nafasi kutakuwa na nafasi moja maalumu kwa wanawake, hivyo akina mama ambao walishawahi kucheza soka wajitokeze kwa wingi kuchukua fomu.
No comments:
Post a Comment