Na Shaban Mbegu
TIMU ya vijana ya Simba, jana imetinga nusu fainali ya michuano ya vijana ya Uhai Cup kwa kishindo, baada ya kuwafunga JKT Oljoro 5-3 katika mchezo wa robo fainali uliofanyika
Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Simba itakutana na Toto African ambayo nayo jana iliifunga JKT Ruvu 4-2 katika mchezo mwingine wa robo fainali, uliofanyika Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Kutokana na matokeo hayo Simba, itakutana na Toto Africa katika mechi ya nusu fainali, ambayo inatarajiwa kuwa ya aina yake itakayochezwa keshokutwa.
Timu hizo katika hatua ya makundi Simba ilinyukwa bao 1-0 na Toto, hivyo matokeo hayo ndiyo yanaufanya mchezo huo kuwa mgumu, kwani kila moja itataka kushinda ili kucheza fainali.
JKT Oljoro ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao, dakika ya pili kupitia kwa Hans Mwaisela ambaye aliachia shuti kali, lilogonga mtamba wa panya na kutinga nyavuni.
bao hilo lilizua mjadala, baada ya wachezaji wa Simba kulikataa kwa madai kuwa halikuingia, lakini mwamuzi wa akiba alionesha kuwa lilivuka mstari.
Simba baada ya kufungwa bao hilo, walitulia na kuanza kulisakama lango la wapinzani wao, mashambulizi hayo yalizaa matunda dakika ya 13, bao lilofungwa na Miraji Athumani akiunganisha krosi ya Frank Sekule.
Bao hilo lilionekana kuwashtua Oljoro, ambao walianza kucheza bila ya mpangilio na kuruhusu Simba, kutawala mchezo kwa asilimia kubwa.
Athumani ambaye jana alikuwa mwiba kwa Oljoro, aliipatia Simba bao la pili dakika ya 33 kwa penalti baada ya Hamud Habib kuchezewa rafu.
Simba ilipata bao la tatu dakika ya 51 lililofungwa tena na Athuman baada ya kukimbia na mpira winga ya kulia na kuachia shiti kali lilojaa wavuni.
Oljoro walipata bao la pili kwa njia ya penalti dakika ya 66, kupitia kwa Idd Hussein baada ya Omari Kheri, kushika mpira akiwa ndani ya eneo la hatari.
Baada ya kufungwa bao hilo Simba walizidisha mashambulizi na kuandika bao la nne dakika ya 72 ambalo beki wa Oljoro, Adeyun Seif kujifunga akiwa katika harakati za kuokoa.
Simba waliandika bao la 5 dakika ya 76 kupitia kwa Rashid Mkoko aliyeingia kuchukua nafasi ya Athumani.
No comments:
Post a Comment