21 November 2011

Mbunge aishukia CCM

 *Asema muswada waliopitisha unawagawa Watanzania
*Ahoji uhalali wa NEC kusimamia kura za maoni
*Askofu aonya wanaopotosha kuhusu mchakato huo


Na Mwandishi Wetu

SIKU chache baada ya Bunge kupitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2011, Mbunge wa Kigoma Kusini, Bw. David Kafulila (NCCR-Mageuzi), amesema
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake, hakina dhamira ya kushirikisha Watanzania wote ili watoe maoni yao juu ya katiba wanayoitaka.
Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Bw. Kafulila alisema kinachopingwa na vyama vya upinzani pamoja na asasi za kiraia si wazo au dhana ya katiba mpya.

Alisema wanachopinga ni mchakato unaotumika kupata katiba mpya ambapo Aprili mwaka huu, muswada huo ulipelekwa Bungeni ukiwa katika lugha ya Kingereza pamoja na kasoro nyingine hivyo walishauri ukafanyiwe marekebisho na kutafsiriwa kwa Kiswahili.

Aliongeza kuwa, kilichotokea baada ya muswada huo kufanyiwa marekebisho na kurudishwa bungeni, walitegemea kuona muswada huo utasomwa kwa mara ya kwanza ili umma upate nafasi ya kuujadili na kutoa maoni yao.

“Kwa mujibu wa kanuni, muswada ukisomwa kwa mara ya kwanza, umma utapata nafasi ya kuujadili na kutoa maoni yao lakini ukisomwa kwa mara ya pili, wananchi hawawezi kupata fursa ya kutoa maoni yao, ndicho kilichotokea,” alisema Bw. Kafulila.

Alisema Watanzania wanapaswa kushirikishwa kuunda muswada huo tangu mwanzo ili kufikia katiba wanayoitaka sasa kama wameshindwa kushirikishwa katika msingi, upo uwezekano wa kujenga nyumba mbovu.
Bw. Kafulila alisema hoja ya kutaka muswada huo usomwe kwa mara ya kwanza ni kutoa fursa kwa umma ili uweze kutoa maoni yao.

“Rais Jakaya Kikwete angepoteza nini kama muswada huu ungesomwa kwa mara ya kwanza? nini alichopata baada ya muswada huu kupitishwa na wabunge wa CCM, muswada huu ulipaswa kupitishwa kwa masikilizano bila kujali itikadi.
“Kama viongozi tunashindwa kusikilizana katika katiba upo uwezekano wa Taifa kupasuka, muswada huu una kasoro nyingi, Rais Kikwete anaonekana kuwa na nguvu kuliko Bunge la Katiba kwa kurekebisha maudhui ambayo anadhani yanafaa, Tume ya Uchaguzi ambayo inapewa jukumu la kusimamia kura za maoni, imepoteza imani kwa umma.
“Taasisi za dini, jumuiya za kiraia na Vyuo Vikuu vitateuliwa na Rais kuingia katika Bunge la Katiba badala ya kuteuliwa na taasisi zao, kimsingi CCM na Serikali yake wameteka mchakato huu na watakuwa kwenye nafasi ya kuamua wanachotaka,” alisema.

Aliongeza kuwa, katika muswada huo sehemu kubwa imezingatia muafaka kati ya watawala wa Serikali ya Zanzibar na Muungano badala ya kuzingatia muafaka kati ya walawala na watawaliwa.
Alisema msingi wa katiba sio kwa ajili ya watawala wa nchi hizo ili waweze kuelewana jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa Taifa kwani CCM na serikali yake imeamua kubeba mchakato huo peke yao.
Bw. Kafulila alisema ni jambo hatari kuweka rehani mchakato wa

katiba mpya mikononi mwa chama kimoja kwani katiba hiyo ni kwa ajili ya Watanzania wote.
Alisema watu wote waliopo katika vyama vya siasa hawazidi asilimia 10 ya Watanzania wote sasa mchakato wa katiba unapoamuliwa na chama kimoja ni jambo hatari sana.

Aliongeza kuwa, kama Rais Kikwete atasaini muswada huo, NCCR-Mageuzi itawashauri wadau wa demokrasia waliopo katika vyama na wasio wanasiasa, waunganishe nguvu ili kutengeneza katiba wanayoitaka Watanzania.
“Kama tutatekeleza mkakati huo, mwisho wa siku tutapata katiba tunayoitaka, kama mchakato wa Serikali hautakuja na katiba ya namna hii, tutawashawishi Watanzania wapige kura ya kuikataa,” alisema.
N
aye Heckton Chuwa kutoka Moshi anaripoti kuwa, Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi mkoani Kilimanjaro, Muhashamu Isaack Amani, amewaonya wanaopotosha umma kuhusu mchakato wa Katiba Mpya kuwa watakuwa wanajihukumu wenyewe iwapo malengo ya mchakato huo hayataenda kwa matakwa ya wananchi wote.
Askofu Amani alitoa onyo hilo jana wakati wa Ibada maalum ya maadhimisho ya Sikukuu ya Kristu Mfalme yaliyoenda sambamba na Ibada maalum ya kumshukuru Mungu kwa maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara.
Ibada hiyo ilishirikisha majimbo Katoliki yote manne ya Kanda ya Kaskazini ya Same, Mbulu, Jimbo Kuu la Arusha na wenyeji jimbo la Moshi.

“Mungu ametupa nafasi ili tushiriki zoezi hili muhimu na la kihistoria, kwa yeyote awe ni kiongozi wa serikali, vyama vya siasa au ngazi yoyote ya uongozi ambaye atapotosha dhana halisi ya mchakato huu atakuwa anajihukumu mwenyewe, zoezi hili ni muhimu na ndilo litaamua hatma ya nchi yetu kwa miaka 50 ijayo”, alisema Askofu Amani.
Alitoa wito kwa waumini na wananchi wote kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika mchakato huo badala ya kukaa pembeni na kuweka wazi kuwa kufanya hivyo ni udhaifu ambao utakuja kuwa majuto ya baadaye.
Alitoa wito kwa watanzania kutumia maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara kutathmini yote yaliyofanyika na kujifunza kutokana na makosa yaliyofanyika katika kipindi hicho ili kuepuka kuyarudia katika kipindi cha miaka 50 ijayo.

“Kwa sisi tulio hai leo hii tunapoadhimisha miaka 50 ya uhuru wetu hatuna budi kujenga tabia ya uadilifu ili kufungua njia kwa vijana wetu ambao ni wadogo na wale watakaozaliwa kwa ajili ya Tanzania bora ya miaka 50 ijayo” alisema. Aliwataka viongozi walafi na wenye uchu wa madaraka kuacha tabia hizo zinazowakandamiza wanyonge wasioweza kujitetea hata wakionewa na kutaka uhuru wa miaka 50 uliopo usiwe wa bendera badala yake uwe wa kweli unaowanufaisha wananchi wote badala ya watu wachache.

“Ulafi si kwenye chakula na vinywaji tu bali kwenye uongozi haya pia yapo, wako viongozi ambao wanaendekeza ulafi na ufisadi mambo yanayowanyima wananchi haki zao za msingi,” alisema.
Askofu Amani aliwataka viongozi kumuiga Mwokozi wa Ulimwengu Yesu Kristu aliwajali wanyonge na kuwatafuta walikokuwa ili awape kheri na matumaini katika maisha yao mapya.

16 comments:

  1. Kafulila unataka umaarufu kupitia Chadema lakini ole wako waulize CUF walikuwa maarufu sana lakini waliponzwa kuachiana majimbo na Chadema. Namuunga mkono Askofu huyo kwani Watz watakaokaa kando watakuwa wamepoteza fursa muhimu wa kujadili mustakbali wa nchi yao. Hapo watu wanatafuta umaarufu tu lakini katiba ni ya wananchi na si ya wanasiasa,hasa hawa wakiafrika ni wezi,manyangaau ambao wanajilimbikizia mali na marupurupu kwa kuwalaghai wananchi. Wananchi shirikini mchakato wa katiba mpya na mtoe maoni yenu hao wanasiasa wanaangalia maslahi yao tu

    ReplyDelete
  2. Kumlaumu Kafulila kwa hili ni kutomtendea haki. Kafulila ana mawazo yake na ana haki ya kuwa na msimamo kulingana na anachokiamini. Kulingana kwa mawazo ya Kafulila na yale ya CHADEMA si dhambi bali ndiyo ukweli unaoonekana kwa kila upande na ni haki Kafulila ausimamie, autetee na kuulinda. Hongera Kafulila na CHADEMA pia

    ReplyDelete
  3. watanzania tusali kila mtu na iman yake hawa wanasiasa kila mmoja na maslahi yake na katika zoezi tushiriki kikamilifu

    ReplyDelete
  4. ndugu zangu watanzania hi nchi ni yetu sote, kwanini tusijadili mchakato nzima toka mwanzo hadi mwisho? mbona huwa tuna wachagua? tushilikisheni jamani. hayo mawazo ya askofu si wakati wake. tushilikisheni

    ReplyDelete
  5. Nchi ni yetu sote lakini wengine wanajifanya ni wenye nchi hii zaidi. Angalia, sisi Watanganyika kwenye mambo yasio ya muungano wazanzibar pia watayashughulikia lakini ya kwao sisi haturuhusiwi kuyashughulia. Hapo kuna utata. Chazanzibar ni cha wazanzibar cha Tanganyika ni cha watanzania hiyo haiwezekani

    ReplyDelete
  6. Hiki kinachotujia ni kile ambacho kila siku tunajaribu kujionya kuwa tusivunje amani,lakini naomba niwaeleze kwamba ya rais kikwete na chama chake cha CCM kuwapuuza yvama vingine na makundi mengine ya watanzania kwa kejeli na hoja dhaifu na za kitoto ndicho kinachopelekea amani ya nchi kuvunjika.hivi tuseme hawa watu hawalioni hili?au ndiyo tuseme wamelemewa na nchi au wana laana.Acheni mashindano ya kitoto nchi hii ni mali ya wote,tusikilizane tujenge nchi pomoja.

    ReplyDelete
  7. what kafulila is doing is damn RIGHT!!!HE IS NOW A PUBLIC FIGURE AND IS PERFOMING HIS DUTY!!!! WACHA KUMTISHIA!

    ReplyDelete
  8. Mh.Kafulila welldone,nilikuwa sijuwi msimamo wako.Nimekuelewa vizuri sana ninakupa Bigup.

    ReplyDelete
  9. Acha niwambie kila mara nawambia sikio la kufa halisikii dawa,mtoto wakikwele haoni shida ,na aliyepinda hataki kunyooka,na viongozi wengine ufisadi wao wanaona hakuna tatizo wakati jambo liko wazi.Sijui nchi yetu hii imelaaniwa au vipi sijui.Mbona wewe kikwete huoni na watu wako hao kama kuna shida,???Tulia utaona yatakayotokea mwaka 2015 ktk uchaguzi.Nawapa pole sisi ccm.

    ReplyDelete
  10. tumeishachoka na mambo yenu ya siasa sisi mchakato wa katiba tutaenda kuchangia hamjalazimishwa andamane mpaka mwisho tupo wengi tu hatupigi kura wala hatutaki ushenzi wowote wa siasa wala uchafu wa vyama ukizingatia hakuna atakae leta miujiza wala unafuu hapo mnapoteza muda wenu bure badala ya mtukupambana na maisha yako mimi hata ukinipa uwaziri sintamsaidia mtu yeyote zzaidi ya familia yangu nikimaliza familia nitaenda kwa marafiki na majirani basi hiyo ndio mfumo wetu wa afrika na tutauendeleza

    ReplyDelete
  11. si vibaya mtu kueleza hisia zake na kumsikiliza, pima hoja zake na zako je ni zipi zenye nguvu na tija? tabia ya watu wengine hupenda kukosoa lakini hawana mawazo mbadala.
    wanasiasa ni sehemu ya jamii na michango yao ni muhimu kwanza wanachangia kwa kiasi kikubwa mno kuamsha na kuielemisha jamii kuhusu taifa lao na haki zao za kikatiba kupitia mikutano ya hadhara na vyombo mbalimbali vya habari, wasipuuzwe hata kidogo kuingizwa kwenye mchakato wa katiba.

    ReplyDelete
  12. Mr Kafulili u are right forget about those useless pipo who dont have an independent mind, They have to wait for Kikwete and batch of CCM MPs to lie to the Tanzanians.We are tired of CCM and its batch of crooks,We dont trust CCM neither the president,
    We want a pipo driven constitution not CCM one.Remember tanzanians are wiser today than yesterday

    ReplyDelete
  13. CCM inao wabunge wengi tu; yaani hata mbunge mmoja kati yao hakuna anayeona kasoro ya walichokifanya bungeni kuhusu mswada wa katiba mpya walioupitisha?

    ReplyDelete
  14. tanzania ni yetu sote;kwani baadhi ya watu wanaona ni mali yao peke yao?mbunge anapomwomba waziri mikuu avitumie vyombo vya dola kutoa mkongoto kwa asasi za kiraia/jukwaa la katiba;anajua jukumu lake ndani ya bunge.tunahitaji kuvumiliana na kuheshimiana na kutojiona kwamba kitendo cha kuwa bungeni basi una akili nyingi kuliko wote.sikiliza,chambua,eleza dosari unazoziona na mbadala makini.hatujawatuma kwenda kutangaza mkongoto kwa watu.acheni sheria zichukue nafasi yake.bunge lisiwe la kutuhumu kuchunguza,kusikiliza kesi na kuhukumu.

    ReplyDelete
  15. Kafulila unapaswa kufahamu kuwa unapozungumzia suala la Bunge unazungumzia umma wa watanzania, wabunge wengi wa CCM, kwa tafsiri rahisi ni wingi wa watanzania waliowachagua. Hivi unawashambulia watu wa CCM au wananchi waliowachagua? Usije ukawa unazungumzia democrasia katika msimamo wa Udikteta. Angalia usije ukatukana watanzania walio wengi. waliowachagua hao wabunge wa CCM.

    ReplyDelete
  16. Kafulila unapaswa kufahamu kuwa unapozungumzia suala la Bunge unazungumzia umma wa watanzania, wabunge wengi wa CCM, kwa tafsiri rahisi ni wingi wa watanzania waliowachagua. Hivi unawashambulia watu wa CCM au wananchi waliowachagua? Usije ukawa unazungumzia democrasia katika msimamo wa Udikteta. Angalia usije ukatukana watanzania walio wengi. waliowachagua hao wabunge wa CCM.

    ReplyDelete