03 November 2011

Tenga aziwakia Klabu Ligi Kuu

*Ataka mawazo ya mgomo yafutwe

Na Zahoro Mlanzi

SIKU chache baada ya klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara kutishia kuigomea ligi hiyo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodgar Tenga ameibuka na kuzitaka ziondoe tishio hilo kwani hayo siyo makubaliano yao.


Pia, amesisitiza Kamati ya Ligi iliyoundwa ambayo ina wajumbe 10 imeshaanza kazi na kwamba Watanzania wasiwe na wasiwasi juu ya hilo kila kitu kitakwenda kama kilivyoadhimiwa katika Azimio la Bagamoyo na kupitishwa na Mkutano Mkuu wa shirikisho hilo.

Akijibu swali Dar es Salaam jana wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari juu ya maamuzi yaliyofikiwa na klabu hizo katika kikao chao walichokifanya, Tenga alisema Kamati ya Utendaji imetekeleza agizo la mkutano mkuu ambao ulitaka iundwe kamati maalum ya kusimamia ligi hiyo.

"Huo si uamuzi wangu binafsi, naomba wadau wanielewe ni uamuzi ambao ulitokana na maadhimio ya klabu zenyewe ambazo mara kadhaa tangu 2007 tulifanya nazo vikao kujadili suala hili na hata katika Azimio la Bagamoyo tulilizingumza pia," alisema Tenga na kuongeza;

"Kama wao wametishia kugoma watakuwa wameenda kinyume kwani hawawezi kutoa masharti na ndio maana nimeamua kwanza kutoa elimu waelewe huku mchakato wa hilo wanalotaka ukiendelea na naomba mijadala iwepo tena mingi juu ya hilo," alisema.

Alisema katika kuhakikisha kamati hiyo inafanya kazi vizuri kama inavyopaswa, ametuma maombi kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuwaandalia semina itakayowasaidia kupata mpangilio wa masoko ili waongoze ligi vizuri.

Aliongeza kwa kutolea mfano wa nchi kama Ujerumani, Sudan, Tunisia, Ivory Coast na Morocco haziendeeshi ligi kwa kutumia mfumo wa kampuni lakini zina maendeleo makubwa katika soka.

Katika kikao cha klabu zinazoshiriki ligi hiyo kilichofanyika Oktoba 21, mwaka huu jijini Dar es Salaam ziliazimia kuigomea ligi hiyo mpaka malimbikizo ya madeni yao yalipwe, TFF isifanywe tena mazungumzo na mdhamini wa ligi hiyo na tayari mchakato wa usajili wa kampuni umeshaanza, hivgo wataendesha wenyewe.

No comments:

Post a Comment