Na Zahoro Mlanzi
WAKATI timu ya taifa (Taifa Stars), ikishuka uwanjani leo kuumana na Chad katika mchezo wa kuwania kutinga hatua ya awali ya makundi ya kufuzu Kombe la Dunia, kocha wa timu hiyo, Jan Poulsen amesema lolote linaweza kutokea katika mchezo huo.
Taifa Stars itashuka katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa na kumbukumbu nzuri ya mchezo wa kwanza, uliopigwa Ijumaa usiku jijini N'Djamena, Chad ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, hivyo kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Akizungumza Dar es Salaam jana katika mkutano na waandishi wa habari, Poulsen alisema wapinzani wao wana timu nzuri licha ya kupata ushindi wa mabao 2-1 ugenini.
“Hatutawadharau kwa kuwa tumewafunga kwao, tutacheza kwa kulinda huku tukishambulia kwani katika mpira wa miguu lolote linaweza kutokea na hii inatokana na Chad, pia kuwa na timu ya ushindani.
“Wakati fulani nilipokuwa nafundisha Denmark, tulikuwa tunaongoza mabao 3-0 mpaka dakika 90 zikimalizika na ndipo zikaongezwa tatu lakini chakushangaza niliposema tayari tumeshinda, kocha mwenzangu alinisihi nisiseme hivyo kwani mpira hauna mwenyewe,” alisema.
Alisema katika mchezo wa kwanza, wachezaji walijituma kwa kushirikiana na ndiyo maana wakaibuka na ushindi huo na ana imani katika mchezo wa leo watazidisha juhudi na kutinga hatua ya makundi.
Naye Kocha wa Chad, Habibu Salehe akizungumzia mchezo huo alisema wamekuja Tanzania kufanya kazi moja tu, kuhakikisha wanaibuka na ushindi na hatimaye kutinga hatua ya makundi.
Alisema walipoteza mchezo wa kwanza kwa kuwa walicheza na timu ambayo kabla hawakuifahamu, hivyo hawatakubali kurudia makosa yaliyotokea nyumbani kwao na amesharekebisha yale aliyoyaona.
Taifa Stars ikifanikiwa kuifunga Chad, itaingia moja kwa moja hatua ya makundi ambapo kundi lao litakuwa na timu za Ivory Coast, Morocco na Gambia zitakazowania kucheza kombe hilo litakalofanyika 2014, Brazil.
Viingilio katika mchezo wa leo ni sh. 2,000 kwa viti vya kijani, sh. 3,000 ni viti vya bluu na machungwa, sh. 5,000 ni viti maalum C, sh. 10,000 viti maalum B na viti maalum A ni sh. 20,000.
No comments:
Post a Comment