15 November 2011

Esperance washangilia ubingwa wa Afrika TUNIS

Tunisia

MFUNGAJI wa bao la ushindi,  Harrison Afful ameimwagia sifa timu yake ya Esperance kwa kutwaa ubingwa wa Afrika, akisema kuwa, ndoto zake zimetimia.

Mshambuliaji huyo kutoka Ghana, alifunga bao pekee katika mechi ya fainali za Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca, wakitoka uwanjani kwa uwiano wa bao 1-0.

timu hiyo maarufu kwa jina la Damu na Dhahabu, sasa itaiwakilisha Afrika kwenye michuano ya Desemba ya Kombe la Dunia ya Klabu.

"Ulikuwa mchezo wangu mzuri, lakini nilifunga, nawashukuru wachezaji wenzangu walioniwezesha kufunga bao," Afful aliiambia BBC.

"Hii ndoto iliyotimia, lakini kazi iliyo mbele yetu ni kubwa kwa sasa," alisema.

"Tunawashukuru mashabiki wetu, kwasababu bila wao, tusingeweza kufanikisha lolote katika soka."

Ni mara ya kwanza kwa Esperance, kutwaa ubingwa wa Afrika tangu mwaka 1994 na umepatikana mwaka ambao Tunisia imefanya mapinduzi ya kisiasa.

"Hii ni siku ya historia kwa Esperance, Nimefurahishwa na watu wa Tunisia, kwasababu wamefanya mapinduzi, na kombe hili ni kubwa kwa nchi na kwa klabu," alisema mshambuliaji Yannick N'Djeng, baada ya mechi.

N'Djeng, hakufanikiwa kutikisa nyavu katika mechi hiyo, lakini amefurahishwa kuwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha timu yao ya Esperance kutwaa kombe.

"Ndiyo, nilikosa nafasi nyingi, lakini ndiyo soka, cha muhimu ni timu. Ni mmoja wa wachezaji wa timu, sikucheza peke yangu."

Esperance, sasa wanatakiwa kujiandaa kusafiri mpaka Japan kwa ajili ya mechi za Klabu Bingwa ya Dunia mwezi ujao.

"Klabu Bingwa Dunia ni kitu kizuri, kila mchezaji anafikiria michuano kama hiyo," alisema N'Djeng.

Esperance ikiwa nchini Japan itakutana na mabingwa wa Ulaya, Barcelona ya Hispania, Santos ya Brazil mabingwa wa Amerika Kusini, Monterrey ya Mexico mabingwa wa Amerika Kaskazini, Al Sadd ya Qatar ambao ni mabingwa wa bara la Asia na Auckland City ya New Zealand.

Timu nyingine, ni mabingwa wa Japan ambao ni wenyeji wa michuano hiyo, atakayepatikana Desemba 3.

No comments:

Post a Comment