*Zaamua kuunda timu moja
Na Amina Athumani
WAPINZANI wa jadi nchini timu za Simba na Yanga, kwa mara ya kwanza katika historia ya soka zimeungana kuunda timu moja, ambayo itacheza na
Asante Kotoko ya Ghana Desemba 11, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mashabiki wa timu hizo kwa mara ya kwanza, watalazimika kuungana ili kuishangilia timu hiyo itakayokuwa imesheheni wachezaji wa nyota wa timu hizo, iliyopewa jina la 'Marafiki wa Uhuru'.
Kwa kawaida mashabiki wa timu hizo, wamekuwa wakizomeana kila zinapokutana katika mechi mbalimbali lakini katika mechi hiyo wanatarajia kuweka tofauti za pembeni na kuungana kuwa wamoja.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya Future Century Limited, ambayo ndiyo inaratibu mechi hiyo kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Helen Masanja alisema mechi hiyo ni maalumu kama maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Alisema timu hiyo itaundwa na wachezaji 24, Yanga ikitoa 12 bora waliosajiliwa na Simba pia itatoa 12.
"Simba na Yanga ndizo zilizofanikisha kupatikana kwa Uhuru wa Tanzania wakati huo, ndiyo maana tumeamua waungane katika kuadhimisha sherehe za Uhuru ambazo kilele chake kitakuwa Desemba 9, mwaka huu," alisema.
Alisema timu hiyo itakuwa chini Abdallah 'King' Kibadeni kama Kocha Mkuu na Kocha Msaidizi atakuwa Fred Minziro, ambao watakuwa na jukumu la kuchagua wachezaji 12 kwa kila upande.
Mratibu huyo alisema tayari wamepata baraka kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) cha kuileta Asante Kotoko nchini, ambayo inatarajia kutua Desemba 9, mwaka huu na itaweka kambi katika Hotel ya Lamada, Dar es Salaam.
Timu hiyo ya Ghana, itakuja na msafara wa watu 40 wakiwemo waandishi wa habari 10, wachezaji na viongozi.
Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Llyod Nchunga alisema ushabiki wao na Simba ni katika dakika 90 za mchezo na si nje ya uwanja, hivyo wanategemea mashabiki wote watakaohudhuria mechi hiyo wataishangilia kama timu iliyoundwa na pande mbili na si kuzomea, wakati mchezaji wa timu moja atakapocheza fyongo.
No comments:
Post a Comment