28 November 2011

RC Mara akumbana na kilio cha maji Bunda

Na Raphael Okello, Bunda

SAKATA la kucheleweshwa kwa mradi mkubwa wa maji unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) mjini Bunda mkoani Mara tangu
bajeti ya serikali ya mwaka 2006/2007 limetinga kwa Mkuu mpya wa mkoa wa Mara Bw. John Tupa.

Mradi huo ambao umekuwa mwiba mkali kwa Mbunge wa Bunda Bw. Stephen Wasira, kutokana na wananchi kupata usumbufu mkubwa kwa kukosa huduma hiyo kwa muda mrefu ulifikishwa kwa Bw.Tupa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda Bw. Francis Isacc. 

Bw. Isacc alimwambia Mkuu huyo wa Mkoa kuwa mradi huo wa maji umekuwa kero na kuzua maswali mengi kwa wananchi na kwamba linahitaji ufumbuzi wa
haraka kuokoa maisha ya wananchi.

Kutokana na hatua hiyo Bw. Tupa katika mazungumzo yake na wananchi katika mkutano wa adhara alisema uchelewaji wa mradi huo unatokana na Benki ya Dunia kuchelewa kuwasilisha fedha za mradi serikalini.

"Ndugu wananchi serikali imedhamiria kukamilisha mradi huu wa maji ili kuwaondolea kero, lakini pia imekuwa ikisuasua kutokana na fedha za benki  ya dunia kutoharakishwa kutokana na mchakato wake kuwa mrefu," alisema Bw. Tupa na kuongeza.

"Pamoja na hayo wakati ninakuja hapa Bunda Mbunge wenu Bw. Stephen Wasira aliniambia kuwa ni kweli mradi wa maji umechelewa kukamilika kutokana na ukosefu wa fedha na kuwataka muwe na uvumilifu," alisema.

Hata hivyo Bw. Tupa aliwaeleza wananchi kuwa tayari fedha zilizopatikana kutokana na bajeti ya serikali imeshanunua baadhi ya pampu za maji, kujenga matanki mawili ya maji pamoja na kuchora ramani ya miundombinu hiyo.

Wakati huo huo mhandisi wa maji wilaya ya Bunda  Bw. Tanu Deule, ametoa ufafanuzi kuwa fedha za mradi wa maji uliotangazwa na Mbunge wa Bunda Bw. Stephen Wasira, mwaka 2006/2007 mjini Dodoma akiwa Waziri wa maji haikuwa kubwa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu na kwamba mahitaji ya maji katika wilaya hiyo inahitaji fedha zaidi.

Bw. Deule alisema hayo wakati akitoa ufafanuzi kwa wanahabari kuhusu malalamiko ya wakazi wa Bunda kuwa serikali ya Rais Jakaya Kikwete ilitangaza bajeti iliyodaiwa kuwa ni kubwa kwa maendeleo ya maji wilayani Bunda lakini fedha hizo hazijafanya lolote huku wakikabiliwa na ukosefu wa maji safi na salama kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment