28 November 2011

Zanzibar Heroes yakaa pabaya

*Yatoka suluhu na Burundi, Zimbabwe yatakata

Na Zahoro Mlanzi

JAHAZI la timu ya Taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes', limezidi kwenda mrama baada ya kutoka suluhu na Burundi
katika mechi ya michuano ya Kombe la Chalenji iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Burundi ndio inaongoza Kundi B ikiwa na pointi nne, ikifuatiwa na Uganda 'The cranes' yenye pointi tatu, Zanzibar Heroes ina pointi moja na Somalia inashika mkia.

Hiyo ni mechi ya pili kwa Zanzibar Heroes kushindwa kutoa raha kwa mashabiki wake baada ya mechi ya kwanza kufungwa bao 1-0 dhidi ya Uganda 'The cranes'.

Kabla ya mchezo huo kupigwa, Zimbabwe ambayo ni timu mwalikwa iliyokuja baada ya Namibia, iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Djibouti katika mchezo ulioanza saa nane za mchana.

Macho na masikio ya timu ya Zanzibar Heroes pamoja na shabiki wao, yataelekezwa kwenye mchezo kati ya Uganda na Somalia ambao unapigwa leo na zaidi watakuwa wakiiombea mabaya Uganda ipoteze mchezo huo ili iwe na matumaini ya kuwaza kusonga mbele.

Katika mchezo wa jana kati ya Zanzibar Heroes na Burundi, Zanzibar ilianza kwa kasi kuliandama lango la Burundi la dakika ya tano, Othman Oman Tamimu alipiga shuti nje ya eneo la hatari lakini lilipanguliwa na kipa Vladmir Niyonkuru na mabeki waliondosha hatari.

Katika kipindi hicho, timu zote zilishambuliana kwa zamu huku kila moja ikifanya shambulizi la kushtukiza lakini washambuliaji wao hawakuwa makini kukwamisha mpira wavuni.

Kipindi cha pili kilianza kama kilivyokuwa cha kwanza, ambapo Burundi iliwachukua dakika nne kulifikia lango la Zanzibar kupitia kwa Kwizera Pierre alishindwa kukwamisha mpira wavuni baada ya kubaki na kipa Mwadin Ali kwa shuti lake kutoa nje.

Zanzibar ilijibu shambulizi hilo dakika ya 53 kupitia kwa Amir Hamad aliyeingia badala ya Makame Hamad, baada ya kubaki na kipa Niyonkuru lakini shuti alilopiga lilipanguliwa na kuwa kona tasa kutokana na pasi Ali Badru Ali.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu lakini Zanzibar itajutia nafasi iliyoipata dakika ya 70 kupitia kwa Amir ambaye pia alibaki na kipa lakini alipiga shuti dhaifu lililotua mikononi mwa kipa na kufanya mashabiki waliokuwepo uwanjani kutaharuki.

Katika mchezo uliotangulia, mabao ya Zimbabwe yalifungwa na Donald Ngoma dakika ya 10 na Amini Qadr dakika ya 73 na kuifanya iongoze Kundi A kwa tofauti ya mabao dhidi ya Rwanda, zote zikiwa na pointi tatu ikifuatiwa na Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) na Djibouti inashika mkia.

No comments:

Post a Comment