28 November 2011

Vijana tafakarini kabla ya kutenda -Manyanya

Na Bryceson Mathias Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Rukwa na Mbunge wa viti Maalum (CCM) Mhandisi Stella Manyanya, ametaka vijana nchini kusaidia nchi yao
kwa kufanya kazi kwa bidii na kutokubali kupotoshwa na hoja za baadhi ya wanasiasa kwa maslahi yao binafsi badala yake watafakari kila wanachoambiwa kabla ya kuchukua hatua.

Pia kiongozi huyo amesema hapokeo mishahara miwili na kwamba kila mtumishi wa umma anayekuwa na nyadhifa mbili huchagua moja tu kulipwa na si yote mawili kama inavyodaiwa.

Akizungumza katika kipindi kinachorushwa na kituo cha televisheni ya Star  cha tuongee asubuhi jana, Mhandisi Manyanya alisema kutokana na hali ya umasikini uliopo nchini kila kijana anapaswa kuongeza juhudi katika uzalishaji na kuepuka kupoteza muda katika malumbano yasiyo na tija.

Mbunge huyo alikuwa akijibu swali la Mwanchuo wa kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Jiji Mwanza (SAUT) Bw. Stephen Daya, alimuuliza swali la sababu za kutojivua gamba kwa kuacha nafasi moja kati ya ubunge na mkuu wa mkoa.

Mbunge Manyanya aliifananisha CCM na mti wa mwembe wenye matunda mbivu ambao kila mtu anaurushia mawe na kuipinga hoja ya kupokea mishahara miwili na kuweka wazi kuwa upande mmoja ulishasitishwa.

Aliwasifu vijana hao kwa hoja na kuwataka pia kutambua kuwa uchaguzi wa CCm mwakani si wa vijana pekee bali ni wa wanaCCM wote wakiwemo wazee hivyo ni vizuri wakavumiliana kwa hoja.

Akihitimisha mjadala huo Bw. Daya aliyejitambulisha kama mwanachama CCM kutoka Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) alimtaka Mhandisi Manyanya kuachia cheo kimoja madai kuwa anapokea mishahara miwili na kwamba hali hiyo hailingani na Katibu wa CCM wa kijiji kulipwa posho ya sh. 5,000 kwa mwezi.

alisema dhana ya CCM kujivua gamba bado haina mashiko kwa wananchi kwa kile alichodai kuwa ni kutafsiriwa na viongozi vibaya.

Alionya chama chake kutokuwa kama mpanda farasi asiyemudu kuiongoza ikamuangusha na kuwataka wazee kuachia ngazi kupisha vijana badala ya kuwaambia hawana uzoefu wakati bado wanang'ang'ania madaraka .

Kijana huyo alienda mbali zaidi na kuweka wazi kuwa kutakuwa na mbivu na mbichi katika uchaguzi mkuu wa chama hicho mwakani.

No comments:

Post a Comment