14 November 2011

PSPF msisitishe malipo ya wastaafu bali elimisheni.

 Na Rose Itono

MFUKO wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) umekuwa ukitoa malipo kwa wastaafu na
tegemezi  kila mwezi lakini umekuwa ukikwamishwa na wanachama kwa kutokwenda kuhakikiwa.

Malipo hayo hutolewa baada ya wastaafu au wategemezi wao kwenda ofisi za mfuko huo kwa ajili ya kuhakikiwa kwa ajili ya kupata malipo.


Hivi karibuni Ofisa Mwandamizi wa PSPF Bw. Victor Luvena alisema mfuko huo uko katika hatua za kutaka kusitisha huduma ya utoaji malipo ya wastaafu kwa mwezi.

Alisema mpango huo wa kusitisha  malipo hayo linatokana na wastaafu pamoja na wategemezi wao kutokwenda kuhakikiwa.

Nionavyo kwa hilo ni vema PSPF ikasitisha mgomo huo badala yake itoe elimu kwa jamii ili iweze kuelewa umuhimu wa kwenda katika ofisi zao kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki.

Nina imani kwamba siyo wastaafu wote ambao wana uelewa juu ya suala la uhakiki ndiyo maana wanakaa bila kwenda kufanyiwa uhakiki.

Kwani ni wazi kwamba kama PSPF  ikifanya hivyo itawaathiri watu wengi hasa ukizingatia kuwa si wastaafu wote hata wanachama wa mfuko wa uelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa wao kuhakikiwa kabla ya kupatiwa malipo yao.

Kwa sababu naamini kuwa si wastaafu wote na jamii kwa ujumla inafahamu umuhimu wa kwenda kuhakikiwa malipo yao kabla ya kulipwa hivyo ni vema ikafanya utaratibu wa kutoa elimu kwa njia mbalimbali ili kila mtu aelewe na kuona umuhimu wa kwenda kuhakikiwa.

Alisema kuwa,mara kwa mara wamekuwa wakifanya uhakiki katika daftari la wastaafu na wategemezi lakini ilionyesha kuwa wengine hawajitokezi.

Pamoja na changamoto zote zinazoukabili mfuko huu kuna haja ya PSPF kuwaelimisha wanachama wao hata kabla ya kustaafu ili kuepuka usumbufu wa aina yoyote.

Kama inavyoeleweka PSPF inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kutolipa mafao ya wastaafu.

Kinachotakiwa ifanye jitihada kuhakikisha inafuata taratibu na kanunui zilizowekwa ili kuwalipa mapema na siyo kusubiri mpaka wastaafu wahamie katika maeneo mengine.

PSPF ifuate utaratibu uliowekwa kwa ajili ya kuwalipa wastaafu hao kama sheria inavyotaka, kwamba kila mstaafu anapaswa kulipwa mafao yake ndani ya siku saba.

Pamoja na PSPF kuanza kuandaa uboreshaji wa utoaji elimu kwa kuandaa vipindi vya redio na televisheni kwa ajili ya wanachama na wadau wake ipo haja ya kuangalia zoezi hilo na kulisimamia ipasavyo ili kuhakikisha linawafikia walengwa wengine  waliopo katika miji na vijiji mbalimbali.

Kama inavyofahamika asilimia kubwa ya watumishi mara baada ya kustaafu hurudi vijijini kwa ajili ya kujishughulisha na shughuli mbalimbali ni vema elimu hii ikawaangalia kwa undani ili waweze kunufaika nao na kupata mafao yao kwa muda unaostahili kwa kuzingatia matakwa na taratibu zilizowekwa na mfuko.

Kwa kufanya hivyo nina uhakika kwamba PSPFitaweza kutoa huduma kwa wastaafu kwa wakati hasa kwa kuzingatia kuwa ofisi za mfuko zimesambaa katika kila mkoa wa Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment