14 November 2011

Ni vita ya mbeya, UVCCM jino kwa jino na Chadema

Na Agnes Mwaijega

UMOJA wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema  kama Jeshi la Polisi litashindwa kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na Chama cha Demokrasia  na Maendeleo (CHADEMA) utachukua jukumu la jeshi hilo kupambana na chama hicho.


Pia umesema unalaani vikali vitendo hivyo na kusisitiza kuwa kama jeshi hilo litashindwa kuwadhibiti watafanya maandamano ya nchi nzima kupinga mwenendo wa chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaama jana, Katibu Mkuu wa UVCCM, Bw. Martine Shigela alisema vitendo vya uvunjivu amani na usalama wa raia vinavyofanywa na CHADEMA vinakwamisha shughuli za maendelo na kuwafanya Watanzania kuishi kwa wasiwasi.

Alisema katika maandamano ambayo wanayaandaa kuyafanya endapo jeshi la polisi litashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo yanalenga kuuelezea umma wa Watanzania historia ya CHADEMA na madhara ya chama hicho katika amani, maendeleo na usalama wa taifa.

Alisema kuwa UVCCM ina uwezo wa kutosha na limejiandaa kukabiliana na CHADEMA kama jeshi hilo litashindwa.

Alisisitiza kuwa wao kama UVCCM wanalaani vikali kitendo cha wafuasi wa CHADEMA kuugeuza mji wa Arusha kuwa kama shamba la bibi na kusema kuwa watahakikisha wanapambana nao.

"Hali inayoendelea nchini hususani mwenendo wa CHADEMA ni mmbaya na unalenga kuvuruga kabisa amani na usalama wa watanzania.

"Tunaliheshimu sana jeshi la polisi lakini sisi kama UVCCM tunatamka wazi kwamba tumechishwa na vurugu za wanachadema na kama litashindwa kudhibiti vitendo vya wafuasi wa CHADEMA sisi hatutakuwa tayari kuwavumilia alisema,".

Bw.Shigela alisema vurugu hizo zinatokana na CHADEMA kushindwa katika chaguzi mbalimbali na kusema kuwa vurugu wanazofanya hususani katika Mkoa wa Arusha zinatokana na Ghadhabu waliyonayo kutokana na kushindwa.

Alitoa mfano kuwa CHADEMA wana hasira na ghadhabu kali kwa sababu walitumia gharama kubwa katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga wakitegemea kuwa watashinda lakini matokeo ya uchaguzi huo yalikuja tofauti na mategemeo yao.

"Unajua CHADEMA wana ghadhabu kubwa kutokana na ukweli kwamba matokeo walivyotegemea katika chaguzi mbalimbali walizopata hawakupata.

"Tena ghadhabu hiyo inatokana na gharama kubwa waliyoipoteza katika chaguzi mbalimbali," alisisitiza.

Aliongeza kuwa CHADEMA walitakiwa kukubali matokeo kwa sababu ndiyo stahili yao na kusema kuwa baada ya kushindwa wangesimamia ilani yao ya maendeleo katika majimbo  na halimashauri walizoshinda.

Vilevile alisistiza kuwa UVCCM inazitambua mbinu na mipango  ya CHADEMA ambayo ina lengo la kuvuruga amani.

Alidai kuwa CHADEMA ni chanzo cha vurugu za wanafunzi wa vyuo vikuu na kusema kuwa hata jana walienda Chuo Kikuu Dar es Salaam kwa ajili ya kuwahamasisha wanafunzi hao kuandamana jambo amablo halikuzaa matunda.

" Leo (jana) wameenda UDSM kuwahamasisja wanfunzi kufanya maandamano baada ya wao kushindwa jana (juzi)," alisema.

Alidai kuwa wafuasi wa CHADEMA wanaendesha shughuli zao bila kufuata sheria za nchi ndiyo maana wanaleta vurugu.

Hata hivyo alisema pamoja na vurugu wanazozifanya wakae wakijua kwamba UVCCM wako macho na hawako tayari kuoana uvunjifu wa amani unatokea katika nchi ambayo inaongozwa na CCM.

Aliongeza kuwa UVCCM ilihangaika kuzitafuta kura na hivyo kusema kuwa hawako tayari kuona wanapokonywa madaraka kirahisi.

"Tutatumia ghasia kudhibiti ghasia kama hawatakuwa tayari kuacha vitendo vyao," alisisitiza.

Hata hivyo aliliomba jeshi la polisi kuchukua nafasi yake kuhakikisha amani ,usalama na sheria zinaheshimiwa na kufuatwa na CHADEMA ili kuweza kuirudisha nchi katika hali ya utulivu.

No comments:

Post a Comment