24 November 2011

Polisi wazuia maandamano

*Wahofia uvunjifu amani, yalipangwa kufanyika J'mosi 
*Wanaharakati kutafuta njia nyingine kufikisha ujumbe

*IGP Mwema asisitiza jeshi hilo halina nia mbaya

Na Benjamin Masese

SIKU moja baada ya wanaharakati kutoka asasi za kiraia zaidi ya 180, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) na Jukwaa la Katiba Tanzania kutangaza kufanya maandamano ya  amani nchi nzima Novemba 26 mwaka huu, Jeshi la Polisi nchini limeyazuia kutokana na hofu ya kuvunjika kwa amani.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, kwa vyombo vya habari, ilisema kutokana na mchakato unaoendelea wa kupitishwa kwa Muswaada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya nchini, amekuwa akipokea maombi ya kufanya maandamano kutoka taasisi mbalimbali nchi nzima yakiwa na malengo tofauti.

Alisema malengo hayo ni pamoja na kupinga muswaada huo na mengine yakiunga mkono jambo linaloashiria kuleta migongano na hatimaye kusababisha uvunjifu wa amani.

Alizitaja taasisi zilizowasilisha maombi hayo kuwa ni pamoja na Jukwaa la Katiba Tanzania ambalo lilitaka kufanya mandamano ya amani nchi nzima kupinga Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya 2011, ambao ulipitishwa na bunge hivi karibuni.
 
Taasisi zingine ni Asasi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao waliomba kufanya maandamano nchi nzima ili kuwaelimisha wananchi kuhusu upotoshaji mkubwa unaofanywa na baadhi ya vyama vya siasa na washirika ili kuvunja amani ya nchi kupitia mwamvuli wa mchakato wa katiba mpya.  

Alisema pamoja na maombi hayo, pia alipokea maombi ya Umoja wa Wanawake Tanzania wa CCM, ambao walitaka kufanya maandamano Novemba 26 mwaka huu, katika Wilaya na mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar.

“Lengo la mandamano ya Umoja wa Wanawake wa CCM ni kuipongeza hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa hivi karibuni, maombi mengine yaliletwa na Taasisi ya Youth Camp, ambao wanapinga mwenendo wa mchakato wa kudai Muswaada wa Katiba na kudai kuwa, hauendani na utaratibu pamoja na utamaduni wa mtanzania,” alisema IGP Mwema.

Aliongeza kuwa kutokana na mwingiliano wa maombi hayo kila taasisi ikitaka kuwasilisha mawazo au hoja zao kwa njia ya maandamano, jeshi hilo limeona kuna kila dalili za kuwepo uvunjifu wa amani.

“Kutokana na hali halisi, tumeona ni vyema tusitishe maandamano yote na kutoa ushauri kwa wahusika watumie njia mbadala ya kufikisha mawazo yao kama walivyopanga jambo ambalo litasaidia kudumisha amani na utulivu wa nchi.

“Uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi umezungumza na taasisi zote zilizowasilisha maombi katika kikao cha pamoja tulichokifanya Makamo Makuu ya Polisi leo (jana0, ambapo taasisi zote zimekubali kuwa, hoja tulizotoa zilikuwa za msingi hivyo wameridhia kusitisha maandamano na kuahidi watamia njia nyingine kuwasilisha mawazo yao ambazo hazitakuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani,” alisema.

Alisema jeshi hilo halina nia mbaya ya kuzuia mikusanyiko au maandamano bali linatekeleza sheria na kanuni zilizopo. 

Aliongeza kuwa jeshi hilo linapopata taarifa ya mikusanyiko au maandamano hulazimika kuzingatia mambo mengine muhimu kabla ya kuruhusu mkusanyiko au maandamano husika.

3 comments:

  1. MAANDAMANO YAPO KAMA ILIVYOPANGA,LAKINI WANAHARAKATI NA VYAMA VYA SIASA HAWATAHUSISHWA.PIA HAYATAKUWA NA SEHEMU MAALUMU NCHI NZIMA.MAENEO YATAKAYOLENGWA NI OFISI ZA SERIKALI NA OFISI ZA CCM KATIKA NGAZI ZA SHINA,KATA,TARAFA,WILAYA,MIKOA NA TAIFA.CCM MMEZIDI KUTUDHARAU WANANCHI.NGOJA TUWAONYESHE MCHEZO AMBAO HAMTOUSAHAU,MAFISADI WAKUBWA.

    ReplyDelete
  2. NAOMBA WATANZANIA TUJIULIZE NA KUJIBU SWALI HILI; JE MTOTO MDOGO AU HATA MTU MZIMA AKILIA AU AKITAKA KULIA UNAWEZA KUMZUIA KULIA? LABDA MTOTO AU MTU MZIMA ANALIA KWA KUWA ANA NJAA AU ANAUMWA TUMBO. UTAMZUIA KULIA AU KUPIGA KELELE? JIBU NI KUMRUHUSU ALIE ILI UJUE ANA TATIZO GANI IKIWEZEKANA UMSAIDIE. WALA SIO KUMZIBA MDOMO AU KUMPIGA. UKIMPIGA ATAZIDI KULIA. AKINYAMAZA ATALIA TENA BAADAE. TAFUTA TATIZO LAKE KWA KUMSIKILIZA NA KUMBEMBELEZA HADI ATAKAPOKUAMBIA TATIZO LAKE NA UMSAIDIE.

    TUWAOGOPE WATU WENYE NJAA AU WENYE UMASKINI WA KUPAMBIKIZIWA. WATAFIKA MAHALI WATAJIONA HAWANA TENA THAMANI MBELE YA JAMII NA HATA MBELE YA MUNGU.

    WAACHENI WATANZANIA WALIE HADI MIDOMO YAO IPASUKE AU SAUTI ZAO ZIFE KWA KUTAFUTA HAKI!

    WAACHE WANANCHI WAANDAMANE KWA AMANI HAKUNA MTANZANIA MWENYE SHIDA ATAKAYEYEMUUMIZA MWENZIE. WATANZANIA WAMECHOKA NA HAWANA NGUVU ZA KUPIGANA. WALIOSHIBA NDIO WENYE NGUVU NA WANA MALI NA NYEZO ZOTE ZA KUCHOCHEA FUJO NA VURUGU.

    UVUNJJIFU WA AMANI NA VURUGU UMEKUWA WIMBO WA WAKUBWA. HATUA YA AMANI NA UTULIVU ILIYOFIKIWA HAPA TANZANIA SI RAHISI KUTOWEKA HATA KAMA VIONGOZI WA VYAMA NA SERIKALI WATAWALAZIMISHA WANANCHI KUVUNJA AMANI ILIYOPO KWA MATAMSHI YA MANENO YAO.

    WATANZANIA TUSIKUBALI KUVURUGWA NA VIONGOZI WA NCHI.SISI WANANCHI HATUTAKI KUUANA. WADOGO HATUNA CHUKI KATI YETU, TUNAISHI KWENYE NYUMBA ZETU KARIBU KARIBU TUNAKULA NA KULIA PAMOJA, TUNAOLEANA N.K. HATUNA MAGETI, MBWA WAKALI AU BASTOLA KWENYE NYUMBA ZETU.TUNAPENDANA NA TUNAISHI KWA AMANI.FUJO IKITOKEA WAKUBWA WANA MAGARI NA MAHALI PA KUKIMBILIA SISI HATUNA. HIVYO HATUNA SABABU ZA KUFANYA VURUGU.

    ReplyDelete
  3. Hatushangai kwa Polisi Kuchukua hatua hiyo kwani tuliitegemea. Siku zote Polisi Tz. ni MAWAKALA WA UONGOZI USIOHESHIMU DEMOKRASIA. MAANDAMANO NI HAKI YA KIKATIBA. Katiba tuliyonayo pamoja ubovu wake inatoa haki hiyo ya msingi, ibara za 18 na 20 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. SALA LA KIBALI HALIPO KISHERIA (KIKATIBA). Taarifa juu ya kusudio la maandamano hutolewa kwa polisi ili watoe ULINZI katika maandamano yanayokusudiwa. Polisi kuzuia maandamano wanavunja Katiba ya nchi ambayo ni mama wa sheria zote. Nguvu ya umma kamwe haijawahi kushindwa mbele ya mitutu, mabomu ya machozi virungu na maji ya kuwasha!

    ReplyDelete