14 November 2011

Ni vita mbeya

JWTZ, Polisi, wapambana na Machinga
*Wafunga mitaa, wachoma moto magari
*Chanzo Kandoro na sera ya safisha jiji 
 






 Na Esther Macha, Mbeya
JESHI la Polisi mkoani Mbeya jana lililazimika kutumia mabomu ya machozi  ili kuwatawanya  wafanyabishara ndogo ndogo maarufu kama (Machinga) kutokana  na kukaidi amri iliyotolewa na uongozi wa Jiji wa kuwataka kuondoka katika maeneo wasiyoruhusiwa kufanya biashara.


Vurugu hizo zilitokea  kuanzia  saa 2.00 asubuhi baada ya machinga hao kuziba njia kwa mawe na kuchoma matairi kisha kujikusanya  vikundi vikundi na kuanza kurusha  mawe kwa askari wa Jeshi la Polisi.

Hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya fujo hizo kuhamia katika eneo la Uyole ambapo barabara kuu kutoka Dar es Salaam zilifungwa kwa kuchoma moto matairi katika barabara hiyo na kuleta adha kwa kubwa kwa wasafiri kutoka Dar es Salaam.

Barabara nyingine zilizofungwa kwa kuchomwa moto na kuleta adha  kwa watumiaji wa barabara hizo nyingine ni maeneo ya Kabwe, Manjelwa, Nanenane, Mtaa wa Kasisi na Soweto.
  
Magari ya abiria yaliyokuwa na abiria kutoka Dar es Salaam na mikoa ya jirani yalionekana yakishusha abiria na kurudi yalikotoka.

Magari kadhaa yalionekana kuzagaa katika eneo hilo yakiwa yamepinduka baada ya kuchomwa moto na watu wanaosadikiwa kuwa ni machinga

Katika vurugu hizo watu kadhaa walijeruhiwa  kwa kupigwa risasi na kukimbizwa katika baadhi ya Hospitali ya Mkoa wa ile ya Rufaa kwa matibabu.

Baadhi ya majeruhi waliopata majereha katika vurugu  hizo ni, Bw. Abel Mwalukali ambaye alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya baada ya kupigwa risasi iliyomjeruhi katika mkono.

Watu wengine waliopata adha hiyo ni mmoja ya waandishi wa mitandao ya kijamii, Bw. Joseph Mwaisango aliyekamatwa na polisi na kuachiwa.

Kutokana na vurugu hizo Kituo cha Polisi cha Uyole kilinusurika kuchomwa moto na wafanyabishara hao

Hali hiyo ilisababisha watu wananchi kujifungia nyumbani  wakihofia kupata madhara kutokana na vurugu hizo.

Askari wa Kikosi cha Kutuliza ghasia walipojaribu kuendeleza mapambano na vijana hao ili wasiendelee na matukio ya uchomaji moto matairi katikati ya bara bara vijana hao walisambaa na kutokomea  kusikojulikana na kisha baada ya muda kuibuka tena  na kuendelea na vurugu.

Katika eneo la Uyole iliendelea kuwa mbaya huku vibanda vya biashara vikiwa vimefungwa na katika eneo la Uwanja wa nane nane katika Banda la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Mateo Queres na Kituo Kidogo cha Polisi cha askari wa usalama barabarani vyote vilichomwa moto.

Wakizungumza na Majira eneo la tukio  wafanyabishara hao walisema hali hiyo ilisababishwa na uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuwataka waondoke pasipo kuwatafutia sehemu nyingine za kufanyia biashara zao wakati siku zote wanauzia maeneo hayo.

Mwenyekiti wa wafanyabishara hao Bw. Patrik Mwasanguti alisema awali Meya wa Jiji la Mbeya Bw. Athanas Kapunga alisema wafanyabishara hao waendelee na biashara zao wakati wanatafutiwa eneo jingine la kufanyia biashara

Wafanyabiashara hao  wamemuomba  Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Abbas Kandoro kutatua tatizo hilo mapema ili kuepusha madhara makubwa kama ambavyo yamekwisha kutokea.

Kuchafuka kwa halia hiyo  kumeatokana na kutokana na Bw Kandoro kuja na sera ya safisha jiji ambayo wakuu wa mkoa wote waliopita walishindwa kuitekeleza.

Wiki  mbili zilizopita alianzisha kampeni hiyo na badaye alitoa ahadi lakini juzi hakutekeleza ahadi yake hiyo na kuwamauru magambo katika jiji hilo kuapambana na wamachinga hoa

Hii ni mara ya pili kwa  Bw Kandoro kukutwa na mkasa kama huo baada katika Mkoa wa Mwanza ambapo wamchinga waliingia mitaani na kupambana na Polisi kwa nia ya kudai maeneo ya kufanyia biashara baada ya ya maeneo waliyokuwa wakifanyia biashara kukatazwa.

Naye Salim Nyomolelo anaripoti kuwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana waligoma kuingia madarasani kwa lengo la kuishinikiza serikali kuwapa mikopo wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na chuo hicho bila ya kupata mkopo.

Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti wanafunzi wa chuo hicho  kwa nyakati tofauti walisema kuwa walifikia uamuzi huo baada ya kuona kuwa wenzao walikosa mikopo ambapo watoto wa matajiri wakipewa.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa mmoja wa wanafunzi wa chuo hicho, Bw. Imani Mosses wa mwaka wa kwanza ambaye anachukua masomo ya Uhasibu alisema kuwa yeye ni mmoja wapo ya waliokosa mikopo lakini chuo kiliwachagua kujiunga na masomo.

Alisema kuwa baada ya serikali kutoa tamko la kutokuwa na bajeti ya kutosha ilibidi ajilipie na kuongeza kuwa anasikitishwa kwa kukosa mkopo ikiwa watoto wa matajiri walipata mkopo.

"Sisi masikini hatupewi mkopo lakini kuna watoto wa matajiri na ushahidi tunao walipewa mikopo, sasa haki ikowapi",alihoji Bw.Mosses

Mwanafunzi mwingine wa mwaka wa kwanza anayechukua masomo ya Uhasibu Bw.Kei Msena alisema kuwa kuna jumla ya wamafunzi 1020 chuoni hapo ambao wanavigezo vyote lakini walikosa kupewa mkopo huku watoto wa matajiri wakiendelea kusoma kwa raha.

Alisema kuwa waliandaa maandamano ya amani kuelekea Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)ambapo walikuja askari wa kutuliza ghasia FFU na kuanza kuwatimua walipokuwa wakidai haki yao.

"Hadi sasa kuna wenzetu 46 ambao wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kuchochea mgomo pindi tunapodai haki zetu," alisema

Hata hivyo wanafunzi hao walisema kuwa mikopo inayotolewa na serikali bado haitoshelezi huku wakidai kuwa serikali iangalie upya.

"Somo linaghalimu sh. milioni 1.5 na serikali unakuta inachangia elfu sitini jambo ambalo kwangu sioni kama msaada," alisema

Hata hivyo gazeti hili lilionana na uongozi wa chuo hicho Prof. Yunus Mgaya ambaye ni makamu wa ushauli wa utawala na sayansi ya majini na kusema kuwa wanafunzi hao waligoma ili kuishinikiza serikali kuwapa mikopo kwa wale waliokosa.

Alisema kuwa sio wanafunzi wote ambao waligoma kuingia madarani na kuongeza kuwa baadhi ya wanafunzi wanaosoma sayansi na ukandarasi walipinga mgomo huo na wanaendelea na masomo.

Alisema mgomo huo uliandaliwa na watu wachache anaojiita wanaharakati ili kuwashawishi wengine kugoma na kuongeza kuwa wanafunzi waliogoma ni wa mwaka wa pili,tatu,na nne ambao wao walishapata mkopo

2 comments:

  1. Naona Kandoro hii kazi ya ukuu wa mkoa imemshinda.Hivi lazima afanye kazi hiyo hiyo tu ambayo imemshinda?.Naona neno busara liko mbali sana na yeye na sijui hata huo uongozi alisomea wapi.

    ReplyDelete
  2. Ni mbumbumbu hana upeo wa kufikiria mambo ya muhimu na athari za kile alichokifanya. Haya ndio matunda ya kupeana madaraka kwa kujuana wakati watu wenyewe hawana uwezo huo, huwezi kuwahamisha watu bila ya kuwatafutia na kuwaonyesha au kuwakabidhi maeneo mapya ya biashara ambayo yatakidhi kile wanachokifanya. la muhimu kandoro hana skills za uongozi ni mjinga asiye na mtazamo wa kile kilichomkuta dar es salaam na mwanza kwani kila anapoenda yy ni kopi na kupesti kila mkoa akipelekwa yy anadili na wamachinga tu na sio kufanya mambo mengine ya msingi katika kuleta maendeleo ya mkoa husika. Jifunze toka nyuma.

    ReplyDelete