17 November 2011

Namba ya simu yatajwa kesi ya Mintanga

Rehema Mohamed

SHAHIDI wa tatu katika kesi kusafirisha dawa za kulevya Godfrey John, inayomkabili Rais wa zamani wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Shaabani Mintanga ametaja namba ya simu ya mtu aliyekata tiketi za ndege za mabondia waliokwenda nchini Mauritius.
John ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni ya Anvelope Travel Agency aliyetengeneza tiketi hizo, alitaja namba hiyo jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mbele ya jaji, Dkt. Fauz Twaib wakati akitoa ushahidi wake mahakamani hapo.

Shahidi huyo alitaja namba hizo kuwa ni 0754-284 887 namba, ambazo kwa mujibu wa ushahidi uliopo mahakamani hapo ziliwahi kutajwa na shahidi wa kwanza katika kesi hiyo Christopha Mtamburukwa, ambaye alikuwa ni Makamu wa Rais wa BFT.

Hata hivyo John, akiongozwa na wakili wa Serikali Prodence Lweyongeza, alisema hawezi kumkumbuka au kumjua mtu mwenye namba hizo kwa kuwa ni muda mrefu umepita na hakujitambulisha kwa jina.

Katika ushahidi wake, Mtumburukwa alisema namba hizo ni za mshtakiwa Mintanga, kwani alidai mahakamani hapo kuwa alikuwa anawasiliana na mshtakiwa huyo kupitia namba hiyo, mara kwa mara wakati wa maandalizi ya safari ya kwenda nchini Mauritius.

Katika hatua nyingine, Mahakama hiyo imepokea vielelezo ambavyo juzi vilikataliwa na upande wa utetezi kwa madai kuwa havikuwa halisi.

Vielelezo hivyo ni tiketi tatu za ndege, ambazo mahakama iliwaamuru wakazifanyie marekebisho.

Katika kesi hiyo ya mwaka 2008, Mintanga anatuhumiwa kukutwa na makosa mawili, ambayo kosa la kwanza ni kula njama ya kusafirisha dawa za kulevya kwenda Mauritius.

Kosa la pili ni kula njama na watu wengine, ambao hawako mahakamani hapo kusafirisha dawa hizo, zenye uzito wa kilo 4.8.

No comments:

Post a Comment