10 November 2011

MWENYEKITI -CHADEMA -ajisalimisha Polisi

Na Queen Lema, Arusha

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe, jana alijisalimisha polisi siku moja baada ya jeshi hilo kutangaza kumtafuta.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuingia Kituo cha Polisi kuhojiwa, Bw. Mbowe alisema taarifa zinazodai kuwa alikimbia si za kweli bali alikuwa katika majukumu mengine ya kikazi wakati mabomu yakipigwa katika Viwanja vya Unga Limited mjini hapa.

Alisema kitendo cha polisi kusema wakati wa tukio la kutawanya wanachadema yeye alikuwepo eneo hilo ni uzushi na amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw.Magesa Mulongo aache kauli za kibabe za kutishia wanachama na viongozi wa Chadema.

Alisema yeye ni kiongozi wa wananchi katika mji wa Arusha mjini ambako chama hicho ndicho kimeshika hatamu na hivyo yeye haogopi polisi wala magereza kwani yupo sahihi na ndiyo maana amejisalimisha.

Bw. Mbowe alisema chanzo mgogoro wa Arusha ni Serikali kukaa kimya kuhusu sakata la umeya wa jiji la Arusha.

Wakati tunakwenda mitamboni Bw. Mbowe alikuwa akiendelea kuhojiwa Kituo cha Kikuu cha Kati (Central) mjini Arusha aloanza kuhojiwa kuanzia tisa mchana.

No comments:

Post a Comment