Na Heri Shaaban
KADA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw. Fred Mpemdazoe, amesema misingi iliyowekwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, iliyozingatia usawa wa kujitegemea na kuiweka nchi katika amani na utulivu imetoweka.
Bw. Mpendazoe aliyekuwa mgombea Ubunge wa Jimbo la Segerea kwa tiketi ya CHADEMA aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea maoni yake kuhusu kile alichokiita kuwa ni uelekeo wa nchi baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere.
Bw.Mpendazoe alisema uongozi wa Mwalimu Nyerere ulizingatia haki usawa na kujitegemea na kwamba kutokana na msimamo huo Tanzania ilikuwa nchi ya amani ya kweli.
"Miaka inavyozidi kwenda baada ya baba wa Taifa kufariki vyama vyetu vya siasa vimeonekana havina maana hata kwa wagombea wake wa nafasi za ubunge na udiwani, wamekuwa wakikamatwa na kusekwa rumande kila kukicha na kushindwa kutoa mchango wao kwa wananchi jimboni,"alidai Bw.Mpendazoe.
Alisema kutokana na uongozi mahiri wa Mwalimu Nyerere watanzania walikuwa wazalendo kwenye nchi yao na waliheshimika duniani kote kwa umoja na mshikamano waliokuwa nao katika masuala ya kitaifa.
Pia Tanzania ilishangaza dunia kutokana na amani iliyokuwepo pamoja na kuwa nchi changa na masikini.
Alisema chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere CCM kilisimamia misingi ya haki, usawa na kujitegemea ambapo chama hicho kilikuwa kilipigania haki za maskini na wanyonge.
Mwanasiasa huyo alishangazwa na uongozi uliopo wa CCM kushindwa kuiweka nchi mahala pazuri na kusababisha kuyumba kwa uchumi na kufanya wananchi wake kuteseka na maisha.
Alikerwa na kile alichodai kuwa ni matukio ya unyanyasaji yanayofanywa na Polisi mkoani arusha kwa wanasiasa akiwemo Mbunge wa jimbo hilo Bw.Godbless Lema.
No comments:
Post a Comment