Na Amina Athumani
MAKOCHA wa kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Boniface Mkwasa na Jamhuri Kihwelu 'Julio' jana
wameshindwa kuchuja wachezaji wa timu hiyo, watakaocheza michuano ya Tusker Challenge Cup kutokana na wote kuwa na viwango vya juu.
Kikosi hicho cha Kili Stars, kinaundwa na wachezaji 28 lakini wanatakiwa kuchujwa ili kubaki 20, kwa mujibu wa sheria za michuano hiyo.
Kili Stars inatarajia kuanza kampeni zake za kutetea ubingwa keshokutwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Rwanda 'Amavubi'.
Wachezaji 20 watakaocheza michuano hiyo, walitakiwa kutangazwa jana lakini makocha hao walishindwa kufanya hivyo.
Awali kocha msaidizi wa timu hiyo Julio, alisema wachezaji wote aliowaita katika kikosi hicho ni wazuri na wenye viwango vya juu, jambo ambalo linawapasua vichwa katika kupata 20 bora watakaounda timu hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Boniface Wambura, alisema kwa mujibu wa makocha hao kikosi hicho kitatangazwa leo, baada ya mazoezi ya asubuhi.
Wachezaji walioitwa Kilimanjaro Stars ni makipa Juma Kaseja (Simba), Deo Munishi (Mtibwa Sugar) na Shabani Kado (Yanga).
Mabeki wa pembeni ni Shomari Kapombe (Simba), Godfrey Taita (Yanga), Juma Jabu (Simba) na Paul Ngelema (Ruvu Shooting).
Mabeki wa kati ni Juma Nyoso (Simba), Said Murad na Erasto Nyoni (Azam) na Salum Telela (Moro United).
Viungo ni Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Ibrahim Mwaipopo (Azam), Nurdin Bakari (Yanga), Mwinyi Kazimoto na Haruna Moshi (Simba), Ramadhan Chombo (Azam), Rashid Yusuf (Coastal Union), Jimmy Shogi (JKT Ruvu Stars) na Mohamed Soud (Toto Africans).
Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Gaudence Mwaikimba (Moro United), John Bocco (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe DRC), Hussein Javu (Mtibwa Sugar), Daniel Reuben (Coastal Union) na Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada).
No comments:
Post a Comment