24 November 2011

Munich, Inter, Benfica zafuzu 16 bora Ulaya

BERLIN, Ujerumani

BAYERN Munich, Inter Milan na Benfica zimefuzu hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kucheza mechi
zao juzi.

Timu ya Ujerumani, Bayern Munich ilipanda juu Kundi A baada ya kushinda mabao 3-1 dhidi ya Villarreal, Inter nayo ilifanya hivyo katika Kundi B, baada ya kutoka sare na Trabzonspor, huku Benfica kwa kutoka sare na Manchester United ilikata tiketi katika hatua ya mtoano ya timu 16.

Franck Ribery aliifungia mabao mawili Bayern, kutokana na juhudi za Mario Gomez, huku Jonathan De Guzman aliifungia bao la kufutia machozi Villarreal.

Napoli imewavuka wapinzani wao Manchester City katika nafasi ya pili, baada ya kushinda mabao 2-1 katika mechi ya Kundi A iliyochezwa Naples, mabao yake yalifungwa na Edinson Cavani.

Sare ya bao 1-1 kati ya Trabzonspor, nayo iliiwezesha Inter kuwa juu katika Kundi B.

Ricardo Alvarez alianza kuifungia Nerazzuri, lakini Halil Altintop  alisawazisha muda mfupi baadaye.

Lille ikiwa ugenini, ilishinda mabao 2-0 dhidi ya CSKA Moscow  na kufanya kundi hilo kila timu kuwa na nafasi sawa, Moussa Sow alifunga bao baada ya Vasili Berezutsky kujifunga.

Kwa mujibu wa Daily Mail, matokeo hayo yamefanya timu zote kuwa na pointi tano, pointi moja nyuma ya Trabzonspor. Lille itacheza na timu ya Uturuki katika mechi yao ya mwisho, wakati CSKA itakwenda Italia kucheza na Inter.

Kundi C linaonekana kuwa gumu, lakini pambano kati ya Manchester United dhidi ya Basle, litakuwa la kufa au kupona kwa United ambayo ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Benfica, katika Uwanja wa Old Trafford.

Basle iliifunga Otelul Galati, mabao 3-2 baada ya kupambana na kutoka nyuma, timu hizo sasa zinatofautiana pointi moja.

Benfica imeweka rekodi ya kutoka sare dhidi ya United na Basle, ina maana wamefuzu bila ya kujali matokeo yao ya mwisho katika mechi yao ya Uswisi.

Real Madrid ambayo ilishafuzu, imeendeleza rekodi yake ya kushinda kwa asilimia 100 katika mashindano hayo, baada ya kuichapa Dinamo Zagreb mabao 6-2 katika mechi ya Kundi D.

Licha ya kuwapumzisha wachezaji wake muhimu, Real iliweza kuongoza kwa mabao 4-0 katika dakika 20, baada ya Karim Benzema na Jose Callejon kila mmoja kufunga mabao mawili, huku Higuain na Ozil na kila mmoja akifunga bao moja.

Dinamo walikuja kupata mabao mawili kupitia kwa Beqiraj na Tomecak.

Ajax alitoka suluhu na Lyon katika mechi nyingine ya kundi D.

No comments:

Post a Comment