Na Amina Athumani
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager, leo imezindua mbio za Bendera ya Taifa ambazo ni sehemu ya Kampeni ya ‘Jivunie uTanzania’ zitakazoambatana na maadhimisho ya sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Uzinduzi huo ulifanyika jana katika makao makuu ya TBL, Dar es Salaam kwa kuwaleta pamoja baadhi ya wanariadha maarufu nchini watakaoshiriki mbio hizo mwishoni mwa mwezi huu na viongozi wa Chama cha Riadha Tanzania (RT).
Akizungumza katika uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui, alisema wanariadha 90, watashiriki mbio hizo.
“Bendera zitakimbizwa na maana halisi ya rangi hizo za bendera ya Tanzania na kutoka kanda ya Ziwa, mbio zitaanzia Mwanza ambapo Bendera ya yenye rangi ya Njano itawakilisha utajiri wa madini yetu, kutoka kanda ya Kati, mbio zitaanzia Dodoma makao makuu ya nchi, bendera Nyeusi itawakilisha rangi yetu waafrika, na kanda ya Pwani bendera ya Bluu itakayowakilisha rangi ya maji, mito na vijito, wataanzia Dar es Salaam,” alisema Nyambui.
Nyambui alisema bendera ya Kijani inayowakilisha misitu na uoto wa asili itatokea katika Jiji la Arusha, ambapo kila kanda itawakilishwa na wanariadha 30.
Alisema wanariadha watakaoshiriki mbio hizo wako katika hali nzuri na wamepangwa vizuri kuhakikisha kuna uwiano mzuri ili kuepuka hali ya kuwa na wanariadha wenye majina makubwa katika kundi moja, na wale wasio na majina kundi lingine.
Naye, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, alisema matayarisho ya mbio hizo yamekamilika, huku akiwapongeza wanariadha hao kwa uzalendo wao kwani kitendo hicho kina umuhimu mkubwa wakati Tanzania Bara inaadhimisha miaka 50 ya Uhuru.
"Bia ya Kilimanjaro ina furaha kuendesha Kampeni ya Jivunie uTanzania iliyozinduliwa Julai mwaka huu, ambapo matamasha mbalimbali yalifanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Kilimanjaro na Mwanza, yakiwa na lengo la kuwakumbusha watanzania wajivunie mafaniko waliyoyapata katika miaka 50 ya Uhuru,"alisema Kavishe.
Alisema baada ya mbio hizo, wanariadha hao watakusanyika mjini Moshi na kuipandisha bendera moja katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, kama alivyofanya Luteni Mstaafu Alex Nyirenda alipoipandisha bendera ya taifa na mwenge wa Uhuru katika kilele cha mlima huo miaka 50 iliyopita.
No comments:
Post a Comment