08 November 2011

BASATA lafurahishwa Ikulu kuwaunga mkono wasanii

Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA), limeelezea kufurahishwa na hatua ya Ikulu kukusanya kazi za sanaa zinazobuniwa na kuzalishwa na wasanii mbalimbali wa kitanzania.
Furaha hiyo imeelezwa mwishoni mwa wiki na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Ghonche Materego, wakati akizindua maonesho ya kila mwaka ya wasanii wachoraji wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Marekani na Sweden yaliyofanyika katika eneo la Nafasi Arts lililoko Mikocheni jijini Dar es Salaam.

“Ikulu yetu imeonesha mfano mzuri sana kwa kuanza kukusanya kazi za sanaa kutoka kwa wasanii mbalimbali wa Tanzania,” alisema Materego.

Hata hivyo, alitoa wito kwa Taasisi, Idara na Wizara mbalimbali za Serikali kuiga mfano wa Ikulu kwa kukusanya na kutumia kazi za wasanii wa nyumbani ili kutanua mianya ya masoko ya kazi zao na kuwasaidia kuongeza vipato vyao.

Materego alisema kuwa, inashangaza kuona ofisi mbalimbali za Serikali zikiwa na kuta zilizo wazi badala ya kupambwa na michoro na kazi za wasanii wa nyumbani kutokana na ukweli kuwa, hiyo ni moja ya njia ya kuwatangaza wasanii na kuwapa fursa ya kuongeza pato.

“Natoa wito kwa wakuu wa Mashirika ya Umma, Idara na Serikali, kuzindua kampeni ya mageuzi katika sekta ya Utamaduni ambayo itawapa ahueni wasanii wetu,” alisema.

Alisema haina maana kuona kuta za majengo yetu zikiwa wazi bila kazi za wasanii.

Alisema ukuzaji wa sekta ya Utamaduni liwe jukumu la kila Taaisi, Idara za Serikali na hata Balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment