22 November 2011

Hakuna atakayewabugudhi wamachinga Mbeya-Kandoro

Na Charles Mwakipesile  Mbeya

MKUU Mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro, amewatangazia neema wafanyabiashara mdogondogo wa mitaani maarufu kama wamachinga kuwa hawatabugudhiwa na mtu yeyote
hadi hapo watakapoandaliwa eneo rasmi kwa shughuli zao.

Pia Mkuu huyo wa mkoa ametangaza kuwachukulia hatua kali wanaosambaza ujumbe potofu ya kuzuka kwa oparesheni ya kusafisha Jiji la Mbeya kwa kuwaondoa wafanyabiashara hao kwa kuwa wanalenga kuvuruga mipango mizuri ya serikali kwa kundi hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake jana, Bw. Kandoro alisema serikali ina mfumo wake wa kufanya kazi kwa kutumia mamlaka zake na kwamba kila eneo ina msemaji na kusisitiza kuwa ngazi ya mkoa yeye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama.

"Ijumaa iliyopita kuna watu walisambaza ujumbe hadi kwenye kituo kimoja cha Redio kuwa siku hiyo Jeshi la polisi lilikuwa limepokea magari manne aina ya Delaiya na mabomu ya machozi kwa ajili ya kuwashambulia  wamachinga, taarifa hizi zilikuwa ni uzushi mtupu na hakuna ukweli juu ya hilo," alisema Bw. Kandoro.

Alisema serikasli haina mpango wa kuwaondoa wamachinga kutokana na ukweli kuwa bado mazungumzo yanaendelea kwa ajili ya kupata sehemu nyingine watakayohamishiwa na kufanya biashara zao kwa uhuru bila kusumbuliwa.

Mkuu huyo wa mkoa alisema serikali inatambua kuwepo kwa wamachinga na ndio maana iliamua kuwajengea jengo katika Mkoa wa Dar es salaam kama hatua ya utekelezaji wa mpango huo katika mikoa mingine kuwawezesha kufanya biashara zao kwa uhuru bila kusumbuliwa na mamlaka za miji.

Katika mazungumzo hayo yaliyojumuisha pia wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa, Bw. Kandoro alisema chombo cha habari kilichohusika kutangaza taarifa hizo kinapaswa kujitathmini na kuona kama kinafuaata maadili au la.

Alisema Jeshi la Polisi wala askari wake hawana mpango wa kuingiza silaha  kwa ajili ya kupambana na wamachinga na kwamba kazi kubwa ya polisi ni ulinzi wa rasi na mali zao.

Aliwata waandishi wa habari kuendelea kutimiza wajibu wao wa kuelimisha jamii kwa maslahi ya taifa na kwa kuzingatia misingi ya maadili ya taaluma hiyo na kutokubali baadhi ya watu wachache kuvuruga tasnia hiyo kwa maslahi yao au ya watu wao.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya Bw. Christopher Nyenyembe, aliweka wazi yeye na uongozi kwa ujumla wamepokea kwa masikitiko kuwepo kwa ukiukwaji wa maadili miongoni mwa redio za mkoa huo na kuahidi kulifanyia kazi kwa kutumia mamlaka yao ili kulinda heshima ya taaluma ya habari nchini.

2 comments:

  1. KANDORO NDIE ALIESABABISHA VURUGU MBEYA NA HATA MWANZA.NCHI NYINGINE ALITAKIWA KUACHIA UONGOZI MAANA HAKUBALIKI NA WATU.

    ReplyDelete
  2. Kandoro, leo unajifanya mwema! unaji-redress ili kumwonesha bana kubwa yako kwamba uko makini! Historia ni chafu kiutendaji, ulipokuwa mkuu wa DSM ulisababisha vurugu za machinga, Mwanza halikadhalika, na leo huko Mbeya umelizua tena... ndiyo tuseme una gundu? Subiri bana kubwa akutafutie kazi nyingine labda akuteue balozi ulaya maana BONGO imeshindikana kuwa kama ULAYA...ULAYA vile!

    ReplyDelete