Na Mhaiki Andrew, Mbinga
TIMU ya soka ya Wilaya ya Mbinga (Mbinga Combain), inatarajia kufanya ziara ya siku nne ya michezo ya kirafiki ya ujirani mwema wa kimataifa na Jimbo la Lichinga nchini Msumbiji, Novemba 15 mwaka huu.
Akizungumza mjini Mbinga juzi, Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu wilayani humo (FAMBI), Peter Mwabu, alisema mchezo huo umeandaliwa ili kujenga na kudumisha uhusiano wa kimichezo kati ya wilaya hiyo na jimbo hilo la Lichinga.
Alisema mahusiano hayo ya kimichezo yatasaidia wananchi wa wilaya hizo kutembeleana na kubadilishana mawazo, kama njia mojawapo ya kudumisha udugu waliokuwanao wazee wa pande zote mbili kabla ya Msumbiji kutawaliwa na Waremo ambao walidumu kwa zaidi karne tano.
Alisema maandalizi ya safari hiyo yamekamilika, zikiwemo viza za kuingia nchini humo, lakini wanasubiri viongozi wa makao makuu ya nchini humo kuwaruhusu.
Alisema timu hiyo itakwenda jimboni humo na wachezaji 15 na viongozi sita, itacheza michezo miwili ya kirafiki na kurejea nyumbani.
Alisema mechi hizo zitapangwa na wenyeji wao baada ya kuwasili jimboni humo, huku akipanga kabla ya kwenda nchini Msumbiji wataomba mechi moja ya kujipima nguvu kati ya Majimaji na Mlale JKT, mchezo ambao utaandaliwa na Ofisi ya Katibu Tawala (DAS) kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment