Na Amina Athumani
TIMU ya kuogelea ya Isamilo ya jijini Mwanza imeibuka washindi wa jumla katika mashindano ya wazi ya kuogelea ya Isamilo Invitational Open Swimming Championship, yaliyomalizika jijini Mwanza, juzi .
Nafasi ya pili kwa washindi wa jumla ilikwenda kwa Stingrays Swm Club ya Dar es Salaam na ya tatu ni Talis ya Dar es Salaam.
Kwa upande wa wachezaji mmoja mmoja waliofanya vizuri kwenye michuano hiyo kwa wenye umri zaidi ya miaka 17 ni Alexandra Belton na Khalid Rushaka, wote wa mwanza.
Wengine ni Niko Kaihua na Stephanie Van Hoppe wa klabu ya Hopac, kwa upande wa watoto chini ya miaka 12 waliofanya vizuri ni Emma Imhoff wa Isamilo Mwanza na Mubanga Pepercorn wa Taliss ya Dar es Salaam.
Akizungumzia mashindano hayo, Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Maselino Ngalioma, alisema michuano hiyo iliwashirikisha waogeleaji 128.
"Wakazi wa Mwanza wameonesha mwamko mkubwa wa kimichezo kwa kujitokeza kwa wingi kwenye viwanja vya shule ya Isamilo kushuhudia mashindano haya yaliyofanyika kwa mara ya kwanza hapa Mwanza," alisema Ngalioma.
Ngalioma alizitaja klabu zilizoshiriki na idadi ya waogeleaji wake katika mabano ni Hopac Swim Club (12), Geita Gold Mines Swim Squard (MVIPS)(9) na Isamilo Mwanza (44), Savannah Plains School Shinyanga (20), Stingrays Swim Club Dar (11), Taliss Dar (15), UDSM Sharks (2) Zanzibar (3) na wengine (12) kutoka sehemu mbalimbali
Ngalioma alisema mashindano hayo yamesaidia kuibua vipaji vipya vya waogeleaji, ambapo Kamati ya Ufundi ya (TSA) Itaviunganisha na timu ya Taifa kwa ajili ya kupata mafunzo zaidi.
No comments:
Post a Comment