Yaichapa 3-0, mashabiki Simba, Yanga wajigawa kuisapoti
*Rwanda hiyo robo fainali
Na Zahoro Mlanzi
TIMU ya Taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars imefufua matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali baada ya kuichapa Djibouti mabao 3-0 katika mchezo wa kuwania Kombe la Chalenji uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Kili Stars sasa ina pointi tatu na kushika nafasi ya pili ikilingana na kwa pointi na Zimbabwe ila zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na Djibouti ikiendelea kushika mkia katika Kundi hilo la A.
Mchezo huo ulitanguliwa na mechi kati ya Rwanda na Zimbabwe ambapo Rwanda imekata tiketi ya kucheza robo fainali ya michuano kwa kushinda mabao 2-0 na kufikisha pointi sita, ikiwa kinara wa kundi hilo.
Pamoja na Stars kupata ushindi huo, bado itakuwa na kazi ya ziada ya kuhakikisha mchezo wao wa mwisho dhidi ya Zimbabwe utakaopigwa Jumamosi haifungwi, ila itasonga mbele endapo itashinda au kutoa sare ya aina yoyote.
Kabla ya mchezo wa Stars na Djibouti haujaanza, wachezaji wa Stars wakati wanapasha moto misuli mashabiki waliokaa upande wa Yanga waliwazomea kwa nguvu huku wale wa kwa upande wanapokaaga mashabiki wa Simba wakiwashangilia.
Hali hiyo iliendelea mpaka walipomaliza mazoezi na kurudi vyumbani na hata mechi ilivyoendelea mashabiki hao waliendelea kuizomea Kili Stars lakini kadri muda ulivyosonga mbele walionekana kugawanyika kwa baadhi yao kuishangilia Stars.
Katika mchezo huo, Kili Stars ilianza kwa nguvu na kuliandama lango la Djibouti na dakika ya kwanza, Thomas Ulimwengu aliifungia Stars bao la kuongoza kutokana na pasi safi ya Ibrahim Mwaipopo.
Stars ilionekana kutakata zaidi eneo la kiungo ambapo dakika ya 37, Mwinyi Kazimoto alifunga bao la pili kutokana na mpira wa adhabu ndogo alioanziwa na Ramadhani Chombo 'Redondo'.
Bao la tatu kwa Stars lilifungwa na Yusuph Rashid dakika ya 84 aliyeingia badala ya Ulimwengu akitumia uzembe wa mabeki wa Djibouti kutookoa mpira wa kurushwa uliorushwa na Godfrey Taita aliyeingia badala ya Said Morad.
Djibouti ilionekana kufanya mashambulizi mara kwa mara kipindi cha pili lakini safu yao ya ushambuliaji haikuwa makini kukwamisha mipira wavuni na hasa kwa kuzidiwa nguvu kwani mipira mingi ilitua miguuni mwa mabeki wa Stars.
Katika mchezo uliotangulia, Rwanda imefuzu hatua ya robo fainali kwa kuichapa Zimbabwe mabao 2-0 ambapo mabao yao yalifungwa na Kagere Medic dakika za 25 na 82.
Rwanda imeshafuzu kwa kujikusanyia pointi sita ambazo zinaweza kufikiwa na Kili Stars au Zimbabwe, kama mmojawapo itamfunga mwenzake katika mchezo kati yao Jumamosi ambao ndio utakaokata mzizi wa fitina.
No comments:
Post a Comment