Akina Mtagwa watakiwa nchini
Rehema Mohamed na Neema Malley
WASHTAKIWA wanaoshikiliwa nchini Mauritius kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya, Petro Mtagwa, Case Ramadhan na Nathalias Charles ambao ni mabondia waliokwenda nchini humo 2008, kushiriki michuano ya ngumi waletwe nchini kwa ajili ya kutoa ushahidi wa kesi hiyo, ambayo pia inamkabili Rais wa zamani wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Shabani Mintanga.
Hatua hiyo imetokea jana ambapo upande wa Jamhuri, umeandika barua kwenda Mauritius kuomba washtakiwa hao, kuletwa nchini kutoa ushahidi wao.
Hayo yalibainishwa jana katika Mahakama ya Kanda ya Dar es Salaam na Wakili wa Serikali, Bi. Stela Machoke mbele ya Jaji Fauzi Twaib, wakati kesi hiyo ilipofika kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa, ambapo upande wa mashtaka uliomba kesi hiyo iahirishwe kwa kuwa hawana mashahidi kwa sasa.
Machoke alidai mahakamani hapo kwa kuwa mashahidi wanaotaka kuwatumia ni washtakiwa wa kesi hiyo ambao wanashikiliwa nchini Mauritius.
Wakili huyo pia aliiomba mahakama hiyo, iwaruhusu mashahidi hao kutoa ushahidi wao kwa njia ya mkutano wa picha ya luninga, kama upande wa Jamhuri utashindwa kuwaleta nchini.
Kutokana na hali hiyo Jaji Twaib, aliahirisha kesi hiyo hadi kikao kijacho cha usikilizwaji, kitakachoanza Februari mwakani.
Jaji Twaib pia aliuamuru upande wa Jamhuri, kuhakikisha shahidi aliyebaki ambaye ni Koplo Abdallah anatoa ushahidi wake katika kikao hicho na kukubali ombi la utolewaji wa ushahidi kwa njia ya mkutano wa luninga.
Awali upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Jerome Msemwa, ulipinga ombi la upande wa Jamhuri la kutaka kesi hiyo iahirishwe kwa kigezo cha kukosa mashahidi kwa kuwa mashahidi waliowaorodhesha wanaishi Dar es Salaam.
Msemwa aliwataja mashahidi hao kuwa ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi, Mkurugenzi wa Michezo Leonard Thadeo, Agness Msengi, Ally Kimwaga, Sajenti Benjamini Mwangata, ASP Fechson Debule, Anjelina Bariangis na Coplo Abdallah.
Katika kesi hiyo Mintanga anakabiliwa na makosa mawili ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 4.8, kwenda Mauritius kwa kushirikiana na watu wengine, ambao bado hawajafikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment